Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Kuelekea bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari kwa mwaka 2023/2024, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa kuboresha huduma za mawasiliano kidigitali ambazo ni kichocheo cha uchumi Kwa jamii.
Dkt.Tulia amesema hayo mara baada ya kutembelea maonyesho ya wizara hiyo na Taasisi zake katika viwanja vya Bunge jana, 2023 maonesho yenye lengo la kuwaonesha wananchi kupitia wabunge wao shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na wizara ikiwa ni pamoja na mikakati yenye ya kuchagiza uchumi.
Amesema TTCL limekuwa mfano kwa makampuni yanayotoa huduma za mawasiliano nchini kwa Ubunifu wa mawasiliano kidigitali ambapo kupitia ubunifu huo kumesaidia kukuza shughuli za kitalii na kuunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuitangaza nchini kwa mataifa mengine.
“Mmekuwa mfano hasa kupitia huduma ya Faiba mlangoni kwako,hii inatufanya kuwasiliana bila hofu, muda wowote na mahali popoote,hata mimi Sasa nitafanya utalii Mlima Kilimanjaro kujionea mtandao huu unavyofanya kazi ,”amesema Spika huyo wa Bunge.
Kuhusu anuani za makazi Dkt.Tulia amewataka wananchi ambao hawajasajili makazi yao kusajili Ili kujua anuani za makazi yao hali itakayo saidia kupata huduma kwa haraka na kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake Meneja biashara wa Mkoa wa Dodoma (TTCL) Leyla Pongwe amesema TTCL imeweza kurahisisha utalii Kwa kufikisha mkongo wa mawasiliano katika kilele Cha Mlima Kilimanjaro ili kuwawezesha watalii kupata mawasiliano Kwa urahisi wakiwa kwenye kilele Cha mlima Kilimanjaro.
Akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga, Meneja huyo ameeleza kuwa huduma ya Faiba Mlangoni zitasaidia kwa kiasi kikubwa matumizi ya internet majumbani na ofisini kwa gharama nafuu.
Amesema kupitia huduma hiyo watalii wamekuwa na Imani na huduma za TTCL na kusaidia kuipaisha Tanzania kimataifa.
“Ili kufikia uchumi wa kidigitali lazima tuwe wabunifu,na Katika kufanikisha hilo tumekuwa wa kisasa kupitia Mfumo wa Faiba mlangoni kwako na kusaidia kuongeza idadi ya watalii,”amesema.