Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesisitiza umuhimu wa msaada wa Marekani katika juhudi za kurejesha amani nchini mwake. Katika hotuba yake, aliomba usaidizi wa dhati wa Washington kuhakikisha kumalizika kwa vita vinavyoendelea.
Wakati huohuo, Rais wa Marekani, Donald Trump, amemkosoa Zelensky, akidai hana “uwezo wa kutosha” wa kuendesha mazungumzo ya amani. Hii inakuja siku chache baada ya kumtaja kama “kiongozi wa kiimla”.
Hali hii inajiri baada ya Trump kuzungumza na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambapo walikubaliana juu ya haja ya kuanza majadiliano ya kumaliza vita vya Ukraine. Tayari, mazungumzo ya kidiplomasia yameanza katika baadhi ya mataifa, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya maafisa wa juu wa Marekani na Urusi yaliyofanyika Saudi Arabia, ingawa Ukraine haikushirikishwa moja kwa moja.
Trump ameeleza dhamira yake ya kusitisha mapigano kwa haraka, lakini kwa mtazamo wa muda mrefu, anaonekana kutaka kupunguza mchango wa Marekani katika mzozo huo. Ikumbukwe kuwa Marekani imetoa msaada wa silaha wenye thamani ya mabilioni ya dola kwa Ukraine.
Aidha, Trump amependekeza kuwa msaada wa Marekani kwa Ukraine unapaswa kuwa na masharti, ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya madini adimu nchini humo kama malipo au fidia ya misaada iliyotolewa. Hata hivyo, Zelensky amepinga wazo hilo, akisisitiza kuwa hawezi kuruhusu “kuuza nchi yetu” kwa namna yoyote ile.
Katika hotuba yake ya video siku ya Ijumaa, Zelensky alifichua kuwa mazungumzo kati ya timu za Marekani na Ukraine yanaendelea, huku akidokeza kuwa makubaliano yanaweza kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
