Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jumatatu ya wiki ijayo, Januari 20, 2025 kuanzia saa 6:00 mchana, siku ambayo Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, ataapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, dunia itabadilika na kuwa na sura mpya. Nasema itabadilika kwa maana kwamba Trump aliuambia ulimwengu wakati anagombea urais kuwa kila mtu atabeba mzigo wake.

Sitanii, Rais Trump aliyepata kuwa Rais wa 45 wa Marekani kabla ya kushindwa na Joe Biden mwaka 2020 katika uchaguzi wa Novemba, ni mfuasi wa Mlengo wa Kulia. Siasa za dunia zina milengo mitatu; Mlengo wa Kulia, Mlengo wa Kushoto na Mlengo wa Kati. Wanasiasa ambao ni wafuasi wa Mlengo wa Kulia kama alivyo Trump, kwao wanajali maendeleo ya vitu na watu, lakini wanapingana na haki za binadamu zisizoleta shibe.

Wanasiasa wa Mlengo wa Kulia wanaamini uhuru usio na mipaka, demokrasia isiyo na mwongozo, na mengine ya aina hiyo ni chanzo cha uharibufu wa maadili, asili, mshikamano wa jamii na maendeleo ya pamoja. Hawa wanaamini ukiisha kufanyika uamuzi, kila mwanajamii anao wajibu wa kuufuata na kuutekeleza, badala ya ‘kupoteza’ muda kwa hoja za kuruhusu demokrasia kuchukua mkondo wake.

Kati ya mambo wanayoyapinga ni pamoja na uhuru uliovuka mipaka. Kwa mfano kuruhusu ushoga na usagaji, maisha ya kiuendawazimu yaliyo nje ya matarajio halali ya jamii, ambapo eti kwa sababu ya uhuru binafsi mtu anaweza kuamua asifanye kazi, asivae nguo au aamke saa 8 usiku na kuwasha vipaza sauti kuhubiri ‘neno la Mungu’, eti anafurahia uhuru binafsi.

Sitanii, Trump amekwisha kusema kuwa kuanzia Januari hii, hakuna shule ya Marekani itakayotoa mafundisho ya ushoga na usagaji kama walivyokuwa wanafanya akina Joe Biden.

Misaada ya kukuza haki za mashoga amekwisha kusema itakoma na askari yeyote aliyepo jeshini nchini humo na ni shoga atapoteza kazi. Amesema dunia haipaswi kupigana vita, badala yake nchi zifanye biashara na kila nchi ipambane kufaidika zaidi.

Trump si muumini wa kutoa misaada. Tutakumbuka katika kipindi alichoongoza Marekani akiwa Rais wa 45, alisema bayana kuwa Afrika inapaswa kusimama kwa miguu yake badala ya kusubiri misaada kutoka nchi zilizoendelea. Suala la vita ya Urusi na Ukraine, ameahidi kulimaliza ndani ya saa 24 atakapoingia madarakani.

Inawezekana baadhi ya watu hawafahamu kabisa vita hii ilivyo na athari kwa nchi za ulimwengu wa tatu na nchi zilizoendelea. Uchumi wa nchi kama Ujerumani uko hoi bin taabani kwa sasa kutokana na vita hii. Walikuwa wanapta gesi kwa bei rahisi kupitia bomba lililotobolewa. Leo wanaagiza gesi ya mitungi kutoka Marekani kwa bei mara mbili na zaidi.

Kwa nchi zetu zinazoendelea ndiyo kasheshe. Urusi ilikuwa inazalisha mapipa ya mafuta ghafi milioni 12 kila siku yanaingia kwenye soko la dunia. Lakini kwa sababu ya vikwazo ilivyowekewa mafuta hayo kwa sasa yamekatazwa kuuzwa kwa nchi zetu. Kampuni za Kimarekani ndizo pekee sasa kupitia nchi mbalimbali zilikowekeza zinauza mafuta kwa bei zitakayo.

Wiki iliyopita katika hali ya kuonyesha kuwa Joe Biden ana shida binafsi na dunia, ametangaza vikwazo vipya dhidi ya kampuni za nchi kama India na China anazodai zinafanya biashara na Urusi, wakati kuna kampuni zaidi ya 300 za Marekani zinazofanya biashara na Urusi na mwaka 2023 zimeilipa Urusi kodi ipatayo dola bilioni 1.2. Marekani wanataka wafaidi wao tu na si nchi nyingine.

Sitanii, ni bahati ya aina yake Trump hataki vita. Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa katika miaka ya karibuni Chama cha Democrat cha Marekani kimekuwa na vinasaba vya kuanzisha vita na kutulazimisha masuala yasiyoendana na maadili yetu. Wakati Trump wa Republican alipoingia madarakani mara ya kwanza, alikuta dunia imejaa hofu ya ugaidi, lakini hadi anaondoka madarakani hofu hii ilipungua sana na alimaliza vita nyingi ikiwamo ya Afghanistan.

Wakati napata faraja kuwa Trump atamaliza vita, kuna upande wa pili wa shilingi. Trump anataka kila biashara inayofanywa Marekani ifaidike. Ndiyo maana leo, kuanzishwa kwa umoja wa BRICS, ambao umeanzisha Benki ya Maendeleo ni tishio kwa nchi za G7. Umoja huu una nchi za Brazil, Urusi, India, China, Afrika Kusini, Misri, Ethiopia, Indonesia, Iran na Falme za Kiarabu kwa sasa.

Umoja huu umeanzisha sarafu yake na nchi wanachama wamekubaliana kutumia fedha za nchi zao kununua bidhaa na huduma bila kulazimika kutumia dola iliyokuwa imefikia hatua ya kuhesabika kama sarafu ya dunia. Jambo hili limewatia hofu kubwa Wamarekani wenye kujitambua wakiona anguko la dola ya Marekani kama zilivyopita za Warumi na Uingereza limewadia.

Sitanii, ni kwa kulitambua hilo Marekani ambayo ina deni kubwa kuliko nchi yoyote duniani kwa maana ya kuwa na deni la zaidi ya dola trilioni 36, kwa sasa inazungumza lugha ya kubana matumizi. Kwa miaka mingi, Marekani wamekuwa wakichapisha noti halali za dola bila kuzifanyia kazi na kutuuzia sisi walimwengu, hivyo tupo kuwatengenezea fedha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, wiki iliyopita akiwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Gilead Teri, wamekutana na wahariri jijini Dar es Salaam na kuzungumza mipango inayotekelezeka sasa. Wameelezea uwekezaji mkubwa uliofanywa, ambao unaakisi kodi kubwa inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kubwa ni uwezo wa Tanzania kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali badala ya zamani ambapo nchi yetu ilizitegemea nchi mbili tu; Uingereza na Kenya. Kwa sasa China inaongoza kwa uwekezaji nchini, kwa kuwa na theluthi moja ya uwekezaji wote uliofanywa. Zinafuatia nchi za Uingereza, Marekani, India, Mauritius, Kenya na Falme za Kiarabu.

Wametumia lugha ya kawaida inayoeleweka. Kwa mfano, kwa sasa vifaa vya ujenzi kama mabati, nondo, saruji, misumari na mengine asilimia kubwa vinatengenezwa hapa Tanzania tofauti na zamani ambapo tuliagiza kila kitu kutoka nje ya nchi. Rais Samia Suluhu Hassan amebadili sheria na sera kuruhusu wawekezaji wazawa kuwekeza hapa nchini kwa kuwapa vivutio.

Ipo mifano mingi, lakini kwa mfano Mtanzania anayewekeza katika hoteli, bidhaa zote anazotumia akiziagiza kutoka nje ya nchi zinasamehewa ushuru wa forodha kwa asilimia 75. Hii imetupatia fursa ya kukuza uwekezaji nchini. Leo hatuagizi tena vitu kama magodoro, miswaki na dawa za meno, viberiti na vitu vingine vingi vya aina hii.

Sitanii, nimeandika makala hii kutabiri kumalizika kwa vita ya Urusi na Ukraine, lakini pia kuna kila dalili kuwa vita ya Israel na Palestina katika Ukanda wa Gaza nayo inakwenda kwisha. Mbali na Trump kutopenda vita, tayari ana mgogoro na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu. Netanyahu alimpongeza Biden katika ushindi ambao Trump anaamini aliibiwa kura, jambo ambalo Trump anaona ni uasi kwake. Tayari ameonyesha dalili za kumaliza vita hii.

Kwa mchanyato wa uwekezaji kutoka nje ya nchi na kwa mkazo wa Tanzania kushirikisha sekta binafsi, ni wazi uchumi wetu unakwenda kupata fursa kubwa chini ya Trump. Sekta binafsi inaendelea kukua. Serikali ya Tanzania inazidi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani na inaendelea kujenga mazingira bora ya kufanya biashara, hali inayoashiria kuwa Trump kuingia madarakani tunaweza kupata neema ya pekee kama nchi na kusimama kwa miguu yetu. Tujiandae kisaikolojia.