Alivyoanza alionekana kama mtoto anayeng’ang’ania kukesha kwenye ngoma ya watu wazima, lakini katika mchakato wa uchaguzi unaoendelea nchini Marekani sasa, Donald Trump anatishia kusambaratisha hali iliyozoeleka kwenye siasa za taifa hilo.
Si mara ya kwanza kwa Trump kujaribu kugombea nafasi kubwa ya uongozi nchini Marekani. Kilicho tofauti sasa ni kasi ya ushindi anaopata kwenye uchaguzi wa ndani wa chama cha Republican zinazoendelea kutafuta mgombea urais atakayepambana na mgombea wa chama cha Democratic kwenye uchaguzi mkuu wa Novemba.
Wamarekani wanao msemo kuwa ni nchini Marekani tu ndiko jambo lolote lisilotarajiwa linaweza kutokea. Si msemo unaotolewa kwa kusifia, bali ni msemo wa kejeli. Ni Marekani tu kwamba mtu ambaye kwenye nyanja za siasa alionekana kama mshereheshaji tu lakini kafanikiwa kupata ushawishi wa kisiasa.
Kwa wale wasiomuunga mkono, Trump anaonekana hafai kuwa rais wa Marekani kwa sababu anaonekana ni mtu ambaye hana uzoefu wa kutosha ndani ya uongozi kuweza kuongoza taifa ambalo lina nguvu kubwa za kijeshi na lenye uchumi unaoongoza kwa ukubwa duniani.
Aidha, ana kasoro ya kutumia mbinu za kuwagawa watu. Siyo tu wapinzani wa jadi kutoka chama cha Democrat wanaamini hivyo, lakini hata viongozi wengi wa chama cha Republican nao wana msimamo kama huu.
Katika historia yake ya kampeni za uchaguzi za miaka ya 1960 chama cha Republican kimewahi kutumia mbinu ya kutafuta kuungwa mkono na wapiga kura wazungu waliopo kwenye majimbo ya kusini kwa kupandikiza chuki dhidi ya Wamarekani weusi. Ulikuwa mkakati usiyo rasmi wa kibaguzi ambao haikutamkwa wazi, lakini ulifanikisha kampeni za siasa na kuongeza kura kutoka kwa wapiga kura wazungu.
Trump anatumia mbinu hizo hizo, ambazo baadhi ya wachambuzi wanasema bado zimeweka mizizi ndani ya chama chake, kwa kujenga chuki dhidi ya wahamiaji kutoka Mexico, na dhidi ya Waislamu. Yale ambayo baadhi ya wagombea wenzake wanayaamini kimya kimya, yeye anayasema wazi na kujizolea umaarufu na uungwaji mkono kutoka kundi la wapiga kura ambalo linashika msimamo kama wake, na ni kundi ambalo linasemekana kwa muda mrefu halijashiriki kwenye uchaguzi. Kwa wagombea wenzake ni sawa sawa na kocha kuingia uwanjani kucheza mechi ya soka akiwa na wachezaji 11 wakati timu pinzani ina wachezaji 20.
Trump anatishia pia uhai wa chama chake kwa sababu anatafuta uungwaji mkono kwa kundi moja la wapiga kura kwa kulishawishi kuwa matatizo yao yanaletwa na makundi mengine ya wapiga kura.
Waislamu siyo sehemu kubwa ya wapiga kura, lakini anaposhambulia wahamiaji wa Mexico anafanikiwa pia kuwaunganisha na kundi kubwa la wapiga kura ambao wanatokea nchi zilizo kusini mwa Marekani na kukipunguzia kura chama cha Republican. Hii ni sababu nyingine inayomjengea uadui wa kisiasa na uongozi wa chama chake. Anavyozidi kufanikiwa kupandikiza chuki dhidi ya makundi haya ndivyo anavyozidi kufanikiwa kuhamishia kura kwenye chama cha Democrat.
Mikakati ya nchi zinazoendelea ya kuhimiza uzazi wa mpango kwa nchi zinazoendelea inajulikana. Watoto wengi wanaleta changamoto kubwa katika kujenga taifa lenye mafanikio. Lakini chama cha Republican kimeng’amua mapema kuwa watoto wengi ni mtaji mkubwa kwenye siasa.
Makundi anayoyashambulia Trump ni makundi ya jamii zenye familia zenye kuzaa watoto wengi zaidi kuliko waungaji mkono wa Democrat wazungu. Kwa namna moja Trump anasambaratisha mtaji wa kisiasa wa muda mrefu wa chama chake mwenyewe. Kwa sababu hii tu, si ajabu kuwa ipo mikakati ndani ya chama chake kuhakikisha kuwa hateuliwi mgombea urais.
Sababu zinatofautiana kwa kiwango kikubwa sana, lakini kwa upande fulani unaweza kufananisha mbio za Trump ndani ya chama chake na mbio za Edward Lowassa za kutafuta nafasi kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi. Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, mikakati ya kila aina inasukwa kuhakikisha kuwa Trump hatafanikiwa kuchaguliwa mgombea urais wa chama cha Republican.
Kwa nchi ambayo baadhi ya viongozi wake hujisifia kuwa ndiyo wenye muundo bora kabisa wa demokrasia duniani, inapaswa kujiuliza swali moja la msingi ambalo nilimuuliza raia mmoja wa Marekani hivi karibuni. Kama Trump anashinda kila anakopita, hii siyo dalili ya kufanya kazi kwa demokrasia? Niliambiwa yanayojiri kuhusiana na umashuhuri wa Trump ni uwezo wa mtu mmoja tajiri kusimamia ajenda yake ya kisiasa bila kuwa na kipingamizi cha pesa. Lakini, kubwa zaidi, aliniambia, wanaomuunga mkono Trump ni wajinga. Ya kwamba hawajui wanachofanya.
Ujinga si tusi, lakini ni neno zito kidogo kuwapachika wapiga kura ingawa haitakuwa mara ya kwanza wala ya mwisho kwa kundi moja la wapiga kura kulipa kundi pinzani jina hilo. Hata kwenye uchaguzi wetu hutokea kuitana majina ya kila aina.
Niliendelea kujenga hoja kuwa hata bila kubishana sana iwapo tunashuhudia ujinga au vinginevyo, bado tunaweza kuwa ndiyo demokrasia yenyewe hiyo; kwenye msafara wa mamba, hata kenge wamo pia. Bado yule Mmarekani hakukubali niliyomwambia. Nilimwambia, basi atakubaliana nami kuwa hata kukubaliana kwetu kwamba hatukubaliani pia nayo ni demokrasia. Hapo tulikubaliana.