Wagombea wa urais wa Marekani, Kamala Harris wa chama cha Democratic na Donald Trump wa Republican wamepambana kwenye mdahalo wa televisheni usiku wa kuamkia leo kiasi miezi miwili kabla ya uchaguzi wa Novemba 5.

Mdahalo huo wa kwanza baina yao umefanyika huko Philadelphia na kuyaweka mezani masuala muhimu ya uchaguzi wa Novemba ikiwemo uchumi, usalama wa mipaka na uhamiaji, sheria za utoaji mimba, mzozo wa mashariki ya kati, vita vya Ukraine pamoja na masuala mengine ya kimataifa.

Suala la kwanza kabisa ilikuwa uchumi ambapo Harris alizungumzia historia ya maisha yake ya kukulia ndani ya familia ya kipato cha kati akiwaahidi wapigakura kwamba mpango wake wa uchumi utasaidia familia za aina hiyo. Amesema atazisaidia biashara ndogo na za kati pamoja na kupunguza kodi kwa familia za kipato cha wastani.

Hoja hizo zilipingwa mara moja na Trump aliyeutalumu utawala wa rais Joe Biden na Harris — ambaye amekuwa makamu wake — kwa kuuharibu uchumi. Trump amesema kiwango cha mfumuko wa bei kwa sasa nchini Marekani kinatisha na kujitapa kwamba alipokuwa madarakani kati ya mwaka 2017 hadi 2021 aliimarisha uchumi wa taifa hilo.

Harris alijibu akisema mpango wa Trump tangu mwanzo hadi sasa ni kuwanufaisha wafanyabiashara wakubwa na ikiwa atashinda itakuwa ni “janga kwa watu wa kipato cha kati na masikini”.