RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump, bado anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa wiki hii kwenye kesi yake ya kumlipa kahaba, baada ya jaji kukataa kusitisha hukumu wakati Trump akiukatia rufaa uamuzi dhidi yake.

Jaji wa Mahakama ya Manhattan, Juan M. Merchan, ameamuru usomwaji wa hukumu hiyo uendelee kama ulivyopangwa siku ya Ijumaa (Januari 10), ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kuapishwa kwa Trump kuwa rais.

Jaji huyo alikataa shinikizo la mawakili wa Trump ambao wamekata rufaa kuitaka mahakama ya rufaa kuifuta hukumu ya awali iliyomtia hatiani mteja wao. Ikiwa hukumu hiyo itasomwa, Trump atakuwa rais wa kwanza kuchukuwa madaraka akiwa ametiwa hatiani kwa uhalifu.

Akiandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, bilionea huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa, amesema endapo hukumu ya Jaji Merchan itasalia kama ilivyo, utakuwa mwisho wa nafasi ya urais kama inavyofahamika sasa.