Rais mteule wa Marekani Donald Trump ametishia kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa muungano wa mataifa tisa wa BRICS iwapo yataunda sarafu pinzani dhidi ya dola ya Marekani.
“Wazo kwamba Nchi za BRICS zinajaribu kujiepusha na Dola huku sisi tukiwa tunatazama imefika mwisho,” Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii Jumamosi.
Nchi zenye nguvu kubwa duniani China na Russia ni sehemu ya muungano wa Brics, pamoja na Brazil, India, Afrika Kusini, Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wakati wa uchaguzi wa Marekani, Trump alifanya kampeni ya kutekeleza ushuru wa wigo mpana.
Ametoa vitisho vya kutozwa ushuru mkubwa katika siku za hivi karibuni.
Ujumbe huu kutoka kwa Trump, ambaye atachukua madaraka rasmi mwaka ujao tarehe 20 Januari, ulilenga Brics, muungano wa mataifa mengi yanayoinukia kiuchumi.
Wanasiasa wakuu nchini Brazil na Urusi wamependekeza kuunda sarafu ya Brics ili kupunguza utawala wa dola ya Marekani katika biashara ya kimataifa.
Lakini kutokubaliana ndani ya muungano huo kumepunguza maendeleo yoyote.