Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito kwa Rais Vladmir Putin wa Urusi kusitisha mashambulizi dhidi ya Ukraine, saa chache baada ya Urusi kuishambulia Ukraine kwa makombora na droni.

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa wito kwa Rais Vladmir Putin wa Urusi kusitisha mashambulizi dhidi ya Ukraine, saa chache baada ya Urusi kuishambulia Ukraine kwa makombora na droni ambayo yametajwa kuwa ni mashambulizi mabaya zaidi katika kipindi cha miezi kadhaa.

Ombi hilo la Trump kwa Putin limekuja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuwataka washirika wake kuiweka Urusi chini ya shinikizo zaidi ili kusitisha mashambulizi yake nchini mwake.

Zelensky alikatisha safari yake kuelekea Afrika Kusini ili kukabiliana na athari za mashambulizi hayo, ikiwa ni tukio la hivi punde zaidi katika wimbi la mashambulizi ya Urusi ambayo yamesababisha vifo vya makumi ya raia.

Katika hatua nyingine, Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff atawasili Urusi wiki hii ambapo anatarajiwa kufanya duru nyingine ya mazungumzo ya kusitisha mapigano na Putin.