Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mzozo wake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy wiki iliyopita, amesema afisa wa Ikulu ya White House.

“Rais Trump amekuwa wazi kuwa anataka amani. Tunataka pia washirika wetu wajitolee kwa lengo hilo. Tunasitisha misaada yetu na kuikagua ili kuhakikisha inachangia katika suluhu,” alisema afisa huyo siku ya Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ikulu ya White House haijaeleza aina na kiasi cha misaada itakayo sitishwa au muda wa kusitisha utadumu kwa kipindi gani.

Pentagon pia haijatoa maelezo zaidi.

Ofisi ya Zelenskiy haijatoa majibu kwa maswali ya Reuters kupitia Ubalozi wa Ukraine huko Washington.

Hatua hiyo imekuja baada ya Trump kupindua sera za Marekani kuhusu Ukraine na Urusi alipoingia madarakani mwezi Januari, na kuchukua msimamo wa urafiki zaidi kwa Moscow.

Haya yanakuja baada ya mabishano makali kati ya Trump na Zelenskiy katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa ambapo Trump alimtuhumu kwa kutoshukuru vya kutosha kwa uungaji mkono wa Washington katika vita na Urusi.