RAIS wa zamani wa Marekani Donald Trump anasema anatarajia kukamatwa Jumanne katika kesi kuhusu madai ya pesa inayosemekana ililipwa kwa nyota wa zamani wa ponografia.
Trump ametoa wito kwa wafuasi wake kupinga hatua hiyo katika chapisho kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii la Truth Social.
Mmoja wa mawakili wa Trump amesema madai yake yalitokana na ripoti za vyombo vya habari kwamba anaweza kufunguliwa mashtaka wiki ijayo.
Iwapo Trump atashtakiwa, itakuwa kesi ya kwanza ya jinai kuwahi kufikishwa dhidi ya rais wa zamani wa Marekani.
Pia itakuwa na athari kubwa kwa kampeni yake ya kuwa mgombea wa Republican katika uchaguzi wa rais wa 2024.
Kwa miaka mitano, waendesha mashtaka mjini New York wamekuwa wakichunguza madai kwamba pesa hizo zililipwa kwa niaba ya Bw Trump kwa nyota wa zamani wa ponografia Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa urais wa 2016.
Daniels amesema alilipwa $130,000 (£107,000) na aliyekuwa wakili wa Bw Trump Michael Cohen kabla ya uchaguzi wa 2016 kama njia ya kunyamazisha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Trump amekanusha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na amepuuzilia mbali kesi hiyo akisema ilichochewa kisiasa.
Ni mojawapo ya kesi kadhaa ambazo mzee huyo mwenye umri wa miaka 76 anachunguzwa kwa sasa, ingawa bado hajafunguliwa mashtaka yoyote na anakanusha makosa katika kila moja.