Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekubali rasmi uteuzi wa kuwania urais kwa tiketi ya Chama cha Republican katika mkutano mkuu uliotawaliwa zaidi na jaribio la mauaji dhidi yake.

Katika hotuba yake ya dakika 90, Trump ametoa ahadi kemkem kwa wapiga kura wake ikiwa ni pamoja na kumaliza migogoro ya kimataifa, kutekeleza operesheni kubwa zaidi ya kuwatimua wahamiaji katika historia ya Marekani.

“Nitamaliza kila mzozo wa kimataifa ambao umeanzishwa na utawala wa sasa, ikiwa ni pamoja na vita vya kutisha kati ya Urusi na Ukraine, ambavyo visingetokea kama ningekuwa rais. Na vita vilivyosababishwa na shambulio dhidi ya Israel, ambalo lisingetokea kama ningekuwa rais.” amesema mwanasiasa huyo wa Republican.

Hotuba ya Trump ya kukubali uteuzi, imeashiria kukamilika kwa mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican ambao ulifanyika kwa siku nne.

Akijivunia mafanikio ya kuaminiwa pakubwa na wakereketwa wa chama hicho, Trump ameshuhudia akiimarisha kwenye uchunguzi wa maoni ya umma tangu mdahalo na rais Joe Biden uliofanyika mwezi uliopita. Kwenye mdahalo huo, Biden alipwaya na tangu wakati huo anakabiliwa na shinikizo kubwa la kumtaka aachie ngazi.

Trump aonesha kuimarika hata kwenye ngome za chama cha Democratic
Kampeni ya Trump imekuwa ikizungumza hata uwezekano wake kupenya katika majimbo yaliyo ngome za chama cha Democratic kama vile Minnesota na Virginia.