Rais wa Marekani Donald Trump amesema leo kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un yuko tayari kukutana naye. Kauli hiyo inaashiria kuwa mkutano wa kihistoria unaopangwa kati yake na kiongozi huyo anayetengwa wa nchi ya bara Asia utaendelea. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Trump ameandika kuwa alipokea ujumbe jana usiku kutoka kwa rais wa China Xi Jinping ukimweleza kuwa mkutano kati yake na Kim Jong Un uliendelea vizuri na kwamba Kim anatarajia kukutana naye. Ameendelea kusema kuwa kwa sasa shinikizo pamoja na vikwazo vya juu vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini sharti vitekelezwe kwa vyovyote vile. Trump ameongeza kuwa yeye pia anatarajia kukutana na Kim. China ilitangaza leo kuwa Kim alizuru nchi hiyo na kukutana na Rais Xi. Kim alisema nchi yake iko tayari kuachana na mipango ya silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.