Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu, wamefanya mkutano wa waandishi wa habari ambapo Trump ametoa pendekezo kwamba Marekani “ichukue udhibiti” wa Gaza, na kuwahamisha watu milioni 1.8 wa Gaza kwenda nchi nyingine za Kiarabu.

Trump amesema baada ya Marekani kuijenga upya Gaza, inaweza kuwa makazi ya “watu wa dunia nzima.”

Alipoulizwa na wanahabari ni kwa mamlaka gani Marekani inaweza kuchukua udhibiti wa Gaza, Trump hakujibu moja kwa moja, lakini amesema anaona kuwa kuna ‘’hati miliki ya muda mrefu.’’

Netanyahu alikubaliana na wazo la Trump na kumuita rais huyo “rafiki mkubwa wa Israel.”

Vile vile Trump alimkosoa mtangulizi wake Joe Biden akidai aliruhusu maadui wa Israel kuwa na nguvu zaidi katika kipindi chake cha miaka minne madarakani.

Mapema, kabla ya pendekezo hilo, msemaji wa Hamas alikosoa pendekezo hilo, akisema ni “mpango wa kuleta machafuko” na akasisitiza kwamba watu wa Gaza hawataruhusu mipango hiyo kupita, bali kinachohitajika ni kumaliza vita.

Benjamin Netanyahu ndiye kiongozi wa kwanza wa kigeni kutembelea Washington wakati wa muhula wa pili Trump katika Ikulu ya White house.