RAIS wa Marekani, Donald Trump, ametangaza uwekezaji mkubwa katika sekta ya akili bandia, ambapo mradi huu unatarajiwa kugharimu dola bilioni 500 katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Trump alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huu utatoa nafasi za ajira laki moja nchini Marekani, na kuwa ni mradi mkubwa zaidi ambao umewekewa historia.

Rais Trump alitangaza hili akiwa ameandamana na wakuu wa kampuni tatu kubwa za teknolojia, akisisitiza kuwa mradi huu utaleta mapinduzi katika teknolojia ya akili bandia.

Mradi huo utaitwa Stargate, na utatekelezwa kwa ufadhili wa sekta binafsi. Trump alisema pia kuwa mradi huu utapanua mipango iliyopo ya kujenga vituo vikubwa vya kuhifadhia na kuchakata data, na kuongeza uzalishaji na uvumbuzi katika sekta hiyo muhimu.