150827102252-donald-trump-july-10-2015-super-169Hofu za kuibiwa kura huwa tunazisikia kwenye nchi ambazo tunaambiwa demokrasia haijakua. Hayo yamebadilika sasa kwa sababu kwenye nchi ambayo tunaambiwa ndiyo mfano bora kuliko yote ya demokrasia, mgombea wa urais ametamka kuhofia kuibiwa kura zake.

Wapigakura wa Marekani wanapiga kura leo kuchagua rais wao wa 45. Donald Trump, mgombea wa urais katika uchaguzi huo- kutoka chama cha Republican, ametamka kuwa ataibiwa kura. Anachuana na Hillary Clinton, mgombea wa chama cha Democratic.

Matokeo ya kura ya maoni yanaashiria kuwa baadhi ya wapigakura wanaamini Trump ataibiwa kura zake. Hata hivyo, ni waungaji mkono wa chama cha Trump ndiyo wanaamini hivyo kwa wingi zaidi, kufikia asilimia 73. Ni asilimia 17 tu ya waungaji mkono wa chama cha Democratic wanaoamini kuwa Trump ataibiwa kura.

Kwa hofu yake, Trump amewapiku hata wale wagombea wetu wa nchi zenye demokrasia changa ambao hulalamika juu ya mchakato wa uchaguzi kwenye nchi zao baada ya matokeo ya uchaguzi. Trump amesema ataibiwa kabla hata hajaibiwa.

Shutuma za wizi wa kura si mpya kwenye uchaguzi wa Marekani. Uchaguzi wa mwaka 1960 uliyomwingiza madarakani Rais John Kennedy kwa ushindi mwembamba mno ulihusisha shutuma za aina hiyo. Baadhi ya shutuma haziwezi kuthibitishwa, lakini yapo maeneo ambako zilipigwa kura nyingi zaidi kuliko za wapiga kura walioandikishwa. Kwenye eneo moja la Jimbo la Texas, Fannin, zilihesabiwa kura 6,138 wakati wapiga kura walioandikishwa walikuwa 4,895 tu.

Hivi karibuni, mwaka 2004, Rais George Bush mdogo alishinda uchaguzi, lakini akaongoza Marekani akiwa na shutuma kuwa alipewa ushindi kwa uamuzi wa mahakama. Kwenye pingamizi za hesabu za kura zilizotokana na hesabu za kura ndani ya Jimbo la Florida, mpinzani wake Al Gore alitaka kuhesabiwa upya kwa kura kwenye jimbo hilo, lakini Mahakama ya Rufani ikatupilia mbali ombi lake. Kuhesabiwa upya kwa kura kungempa Gore ushindi. Kama ilivyokuwa kwa Kennedy, Bush naye alishinda kwa kura kidogo mno.

Kwa hiyo pamoja na kuwa baadhi ya wachambuzi wa siasa za Marekani wanamshangaa Trump kwa kushuku kuibiwa kura, Trump anayo mifano mizuri katika uchaguzi mbalimbali uliopita wa kutetea hofu yake. Tofauti ya Trump na wagombea wenzake kama Nixon dhidi ya Kennedy, na Gore dhidi ya Bush ni kuwa yeye hana aibu ya kusema ana hofu ya kuibiwa. Baada ya uamuzi wa mahakama kumpoka ushindi, Gore alitamka kuwa hakubaliani na uamuzi wa mahakama, lakini anauheshimu. Na yakaishia hapo. 

Inaonekana si ustaarabu hata kidogo kuhoji uhalali wa mfumo wa kupiga kura nchini Marekani. Ni sawa na huku kwetu mwanaume kusema hadharani kuwa anapigwa na mke wake, ingawa tunafahamu kuwa wapo wanaume wengi wanatandikwa vizuri tu na wake zao. Wanaonyanyaswa kijinsia na wake zao wanapaswa kunyamaza kimya. 

Wapiga kura wengi wa Marekani wameonesha kutoridhika na wagombea wote wawili wa uchaguzi wa mwaka huu, na baadhi yao wanasema hawatapiga kura. Wanasema wote hawafai, ila wanapishana kwa sifa zao tu. Wasio Wamarekani wanaofuatilia siasa za Marekani wanafanya hivyo kwa sababu moja kuu ya msingi. Marekani ni taifa kubwa na rais wake anapewa rungu ambalo anaweza kulitumia vibaya dhidi ya raia wa nchi nyingine. Tunachohofia ni kuwa rungu hilo lisiangukie kwenye mikono ya mwendawazimu.

Wanaomuunga mkono Clinton wanasema kuwa Trump ni mwendewazimu na hastahili kuongoza Marekani. Na kwa kweli, katika matamshi yake, tunaona viashiria kuwa inawezekana akishinda tutashuhudia uamuzi wa rais wa Marekani ambao utaongeza hali ya hofu ya wasiyo Wamarekani ya kuchapwa virungu na Marekani. Hiyo hali ipo na imekuwapo kwa miongo mingi tu, lakini inaelekea kuwa ‘Rais’ Trump ataongeza mkong’oto na ubabe.

Tunaweza kuangalia maeneo kadhaa ya sera za Marekani za nje tukatathmini utendaji wa ‘Rais’ Hillary Clinton. Tuna hakika, tofauti na Trump, kwamba hatajenga ukuta kwenye mpaka wake na Mexico kudhibiti wimbi la wahamiaji wa Mexico wanaoingia Marekani. Lakini, kama ambavyo, wengi walikuwa na matarajio kadhaa juu ya awamu ya Rais Barack Obama, ukweli wa awamu unajulikana rais anaposhika hatamu. 

Pamoja na mambo mengine, awamu ya Rais Obama itakumbukwa pia kwa ongezeko kubwa la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya maadui wa Marekani, mashambulizi ambayo yanakadiriwa kuua watu zaidi ya 3,000. Miongoni mwa wanaouawa ni raia wasio wapiganaji. Bush aliidhinisha mashambulizi 50 ya ndege zisizo na rubani. Obama aliidhinisha mashambulizi zaidi ya 500.

Tunachoweza kusema kwa hakika juu ya Rais Hillary Clinton ni kuwa hatufahamu atakuwa rais wa aina gani. Wanaoshabikia tu kwamba atakuwa rais wa kwanza mwanamke, au atakuwa rais wa kwanza ambaye alikuwa mke wa rais wa Marekani wanasahau kuwa atashikilia lile rungu na hatujui atalitumiaje. Baadhi ya waliomfurahia Obama kuwa rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika wamelipata vyema somo hilo kuwa rais wa Marekani hapimwi kwa mwonekano wake.

Tangu mwaka 2002 Marekani imeruhusu waangalizi wa uchaguzi kuwapo kwenye uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, ingawa majimbo 12 ya Marekani hayaruhusu waangalizi hao. Uchaguzi huu utahusisha waangalizi kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na zile zinazowakilishwa na Jumuiya ya Ulaya, na Jumuiya ya Mataifa ya Marekani (OAS).

Kwa hiyo, tunatarajia kuwa hata Trump asiposhinda uchaguzi, hatakuwa na sababu ya msingi kudai kuwa ameibiwa kura. Na tutatarajia kelele zake zififie kadri muda unavyopita. Kama zitakuwapo kelele kutoka maeneo mengine nje ya Marekani hayo tusubiri kutafakari ndani ya miaka minne ijayo.