Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Januari 14, 2025 niliandika makala yenye kichwa cha habari: “Trump kubadili sura ya dunia kuanzia Jumatatu.” Naomba kujinukuu japo aya chache katika makala hiyo. “Jumatatu ya wiki ijayo, Januari 20, 2025 kuanzia saa 6:00 mchana, siku ambayo Rais Mteule wa Marekani Donald Trump ataapishwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, dunia itabadilika na kuwa na sura mpya. Nasema itabadilika kwa maana kwamba Trump aliuambia ulimwengu wakati anagombea urais kuwa kila mtu atabeba mzigo wake.
“Sitanii, Rais Trump aliyepata kuwa Rais wa 45 wa Marekani kabla ya kushindwa na Joe Biden mwaka 2020 katika uchaguzi wa Novemba, ni mfuasi wa Mlengo wa Kulia. Siasa za dunia zina milengo mitatu; Mlengo wa Kulia, Mlengo wa Kushoto na Mlengo wa Kati. Wanasiasa ambao ni wafuasi wa Mlengo wa Kulia kama alivyo Trump, kwao wanajali maendeleo ya vitu na watu, lakini wanapingana na nyingi ya haki za binadamu zisizoleta shibe….
“Sitanii, Trump ameishasema kuwa kuanzia Januari hii, hakuna shule ya Marekani itakayotoa mafundisho ya ushoga na usagaji kama walivyokuwa wanafanya akina Joe Biden. Misaada ya kukuza haki za mashoga ameishasema itakoma na askari yeyote aliyepo jeshini nchini humo na ni shoga atapogeza kazi. Amesema dunia haipaswi kupigana vita, badala yake nchi zifanye biashara na kila nchi ipambane kufaidika zaidi.”

Sitanii, makala hiyo imegusa maeneo mengi. Nianze na hili la ushoga. Marekani chini ya Rais Trump imezuia ushoga. Misaada iliyokuwa inatolewa na taifa hilo kuendeleza ushoga imesitishwa kwa siku 90. Leo napita sehemu mbalimbali nchini na duniani, sijasikia mtu aliyelazwa hospitalini kwamba “ana ugonjwa wa ushoga unamsumbua” hivyo anatafuta tiba.
Hata idadi ya vijana wa “kidole juu” na wasukaji wa nywele hata kwenye miji yetu wamepungua. Ni wazi chama cha Democrat na Joe Biden, walikuwa wanamwasi Mungu. Ilikuwa wanakaribisha Sodoma na Gomora. Chama hicho zamani nilikipenda, lakini nimethibitisha pasipo mashaka, kuwa kila kikiingia madarani vita inachochewa.
Tulishuhudia Biden akizungumza kwa sauti ya kuwaunga mkono mashoga, akidai ni haki za binadamu. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alipinga amri hii na akatunga sheria kuwabana mashoga, wakamwekea vikwazo vya kiuchumi. Tuukatae upuuzi huu. Tanzania Rais Samia alisema “Nchi yetu ni huru, hatutalazimishwa mambo yasiyoendana na mila na desturi za nchi yetu.”
Sitanii, tumeshuhudia Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akiua zaidi ya Wapalestina 47,000 katika vita ambayo Israel ndiye mwanzilishi anayeendelea kuchukua ardhi ya Wapalestina kila kukicha. Maji ya Mto Jordan wanayafunga yasiende kwa Wapalestina, wamewajengea kuta kila kona, kana kwamba Wapalestina wanaishi gerezani. Wanatoka na kuingia katika nchini mwao kwa kuhesabiwa.
Trump alisema kwa sauti ya mamlaka kuwa kabla hajaapishwa, ni lazima Israel na Palestina wawe wamesitisha vita. Kama alivyotaka Januari 18, 2025 wawili hawa walishitisha vita na maisha ya watu yakaokolewa. Trump hata mara ya kwanza mwaka 2017 alipoingia mdarakani, vita ya ugaidi ilikoma duniani. Tulianza kupewa visu na umma vya silver katika ndege badala ya plastiki.
Sitanii, amemwambia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky awe tayari kumaliza vita. Zelensky ambaye miaka iliyopita alikuwa mwigizaji, anataka kuingiza dunia katika Vita Kuu ya Tatu. Kama vile viongozi akili zimewaruka, anawapa amri watoe silaha nchi za Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Poland na wengine wanamwaga mamilioni ya dola kuwapa Ukraine silaha.
Kwa msiofahamu, Ukraine ilikuwa sehemu ya Urusi hadi mwaka 1991 Marekani ilipomtumia kwa ulaghai aliyekuwa Rais wa Urusi wakati huo, Mikhail Gorbachev aliyeingia mpango wa kuiangusha nchi yake. Msambaratiko huo, uliacha silaha za nyuklia katika nchi ya Ukraine. Waliingia mkataba kuwa silaha zote za nyuklia za Urusi zilizoko Ukraine, zitaendelea kumilikiwa na Urusi.
Hadi sasa Ukraine ina silaha za nyuklia zipatazo 1,700 ambazo ni za Urusi. Ikitokea Ukraine ikapata uhuru kamili na kuingia NATO, itakuwa nchi ya tatu duniani kwa kuwa na wingi wa silaha za nyuklia. Hadi sasa, kwa kuhesabu na hizo za Ukraine, Urusi inakiswa kuwa ndiyo nchi yenye silaha nyingi za nyuklia ambazo ukiunganisha silaha za nchi zote duniani hazifikii idadi ya silaha alizonazo Urusi.

Ukiacha kuchezesha takwimu, Urusi inakisiwa kuwa na silaha zaidi ya 7,000, ilhali Marekani inazo 4,000, hivyo ukichanganya za nchi nyingine ambazo zinazo 20 au 50, bado ukijumulisha na Marekani hazifikii idadi ya Urusi. Tramp analifahamu hili. Ndiyo maana amesema kwa miaka mitatu, dunia imeungana dhidi ya Urusi ikiwapa silaha Ukraine, lakini haikushinda hii vita. Tramp anasema vita iishe, nami namuunga mkono.
Sitanii, nawashangaa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer na washirika wao wanaendeleza mapambano. Kwa kutokujielewa wanasema eti wanaikopesha Ukraine, lakini watalipwa deni lao kutokana riba inayotozwa kwenye fedha na mali za Urusi zinazoshikiliwa sehemu mbalimbali duniani. Binafsi ukiniuliza, Tramp anarejesha amani duniani. Kuwanyima silaha Ukraine, ni hatua sahihi ya kumaliza vita. Dunia itakuwa salama tena chini ya Tramp si muda mrefu.
0784 404827