Rais wa Marekani Donald Trump amesema anafikiri kuwa mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky yuko tayari kuliacha eneo la Crimea kwa Urusi kama sehemu ya makubaliano ya amani – licha ya hapo awali Kyiv kukataa pendekezo lolote kama hilo.

Alipoulizwa iwapo anadhani rais wa Ukraine yuko tayari kuachia rasi yake ya kusini, ambayo ilitwaliwa kinyume cha sheria na Urusi mwaka 2014, Trump alijibu: “Nadhani hivyo.”

Trump pia alimtaka Rais wa Urusi Vladimir Putin “kuacha kufanya mashambulizi na badala yake kuketi chini na kusaini makubaliano” ya kumaliza mapigano, akipendekeza hii inaweza kufaikiwa ndani ya wiki mbili.

Alitoa maoni hayo kwa waandishi wa habari baada ya kurejea kutoka Vatican, ambako alifanya mkutano mfupi na Zelensky kabla ya mazishi ya Papa Francis.

Trump alisema mkutano huo “umeenda vizuri” na kwamba Crimea imejadiliwa “kwa ufupi sana”.

Pia alisema kuwa Zelensky sasa alionekana kuwa “mtulivu”, ikilinganishwa na kile kilichoonekana kuwa mzozo wa hadharani kati ya marais hao wawili katika Ikulu ya White House mnamo Februari.

Ukraine imekataa mara kwa mara kufanya makubaliano yoyote ya kimaeneo, ikisisitiza kuwa masuala kuhusu ardhi yanapaswa kujadiliwa mara tu usitishaji mapigano utakapokubaliwa.

Si Zelensky wala Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye amejibu hadharani maoni ya hivi punde ya Trump.

Mapema siku ya Jumapili, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliionya Ukraine kutokubaliana na makubaliano ambayo yanahusisha mapatano makubwa ya ardhi ili kurudisha usitishaji mapigano.

Aliliambia shirika la utangazaji la Ujerumani ARD kwamba Kyiv “haipaswi kufikia pendekezo la hivi punde zaidi la rais wa Marekani”, ambalo alisema lingekuwa “kujisalimisha”.

Waziri wa Ujerumani alisema kuwa Ukraine ilijua inaweza kulazimika kuachana na eneo fulani ili kupata mapatano.