Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Bukoba

Rais mteule wa Chama cha Republican, Donald Trump, si tu ameshinda urais katika uchaguzi uliofanyika Novemba 5, 2024, bali pia ameushinda mkono wa fitina.

Trump baada ya kumaliza urais mwaka 2020, amefunguliwa kesi zaidi ya 100 katika maeneo mbalimbali, nyingi zikijielekeza kutaka kumtia hatiani na ahukumiwe, iwasaidie kumzuia kugombea urais mwaka 2024.

Trump amekuwa Rais wa kwanza Marekani kushitakiwa na kutiwa hatiani, kwa kosa ambalo ushahidi wake Mungu anajua. Mwigizaji Stormy Daniels, anadai mwaka 2016 alilipwa na Mwanasheria wa Trump, Michael Dean Cohen, kuficha kashfa dhidi ya Trump isimwaribie katika kinyang’aniro cha urais. Na kwamba kwa kuificha kashfa hiyo, Trump alishinda urais kwa ulaghai.

Sitanii, katika kesi hii serikali ilimshitaki Trump kwa makosa 34, na yote Wazee wa Baraza wakamtia hatiani. Mwigizaji Stormy, sijui kama alikuwa anaigiza au la, akasema Trump alimbaka kwenye duka la kuuzia nguo. Kwamba alipoingia kwenye chumba cha kujaribia nguo cha duka hilo, Trump alimfuata akambaka, naye aliamua kukaa kimya, ila mwaka 2016 alitaka kuiweke wazi kashfa hii, Cohen kwa niaba ya Trump akamlipa dola 130,000 (Sh milioni 351) kuficha kashfa hii.

Kinachoshangaza, Cohen na Stormy walishirikiana na Serikali ya Rais Joe Biden kuhakikisha kesi inamwelemea Trump. Walitumia ushahidi wa kuungaunga, na Cohen ambaye alikuwa Mwanasheria wa Trump tangu mwaka 2006 hadi 2018 akatokea mahakamani kutoa ushahidi kuwa kweli alitumwa na Trump kutoa fedha hizo kuficha kashfa ashinde urais mwaka 2016.

Huyu Cohen katika hali ya kawaida alipaswa kupimwa akili kama yuko sawa au la. Nasema hivyo, kwani tangu mwaka 2018 alianza kumgeuka Trump. Alianza kwenda mahakamani akikiri kutenda makosa mbalimbali, ikiwamo kusema uongo mbele ya Kamati ya Bunge.

Akazua jingine kuwa Trump alikuwa anakwepa kodi. Mwaka 2019 Cohen alifungwa jela miaka mitatu kwa kukiri kusema uongozi kuwa Trump alikuwa anajenga ghorofa kubwa nchini Urusi.

Sitanii, katika hali ya kawaida ambapo mtu amekwisha kutiwa hatiani kwa kukiri kusema uongo na akafungwa gerezani miaka mitatu, sikutarajia mahakama imwamini asilimia 100 kuwa ndiye shahidi mkuu dhidi ya ‘boss’ wake wa zamani, sasa akithibitisha kuwa mwaka 2016 pia alidanganya au alikataa kusema ukweli kuwa Trump alimlipa Stormy dola 130,000.

Mimi ningekuwa jaji katika kesi hii, huyu Cohen ambaye kila mara anakiri kusema uongo, ushahidi wake dhidi ya Trump kulikuwa na sababu ya kuutilia shaka kuwa nao unaweza kuwa uongo mwingine katika mnyororo wa uongo aliokuwa akiuota kwa muda mrefu. Lakini jambo moja, nadhani wengine hawaufahamu mfumo wa mahakama wa Marekani.

Mahakama ya Upeo ya Shirikisho la Marekani inaendeshwa na majaji tisa. Majaji hawa pamoja na kuwa wanasheria, kwa upande mwingine ni wanasiasa. Majaji ni wanasiasa kwa maana kwamba kabla ya kuteuliwa kwao wanapaswa kuthibitisha kuwa ni wanachama wa chama cha siasa. Wanateuliwa na Rais wa Marekani na wanathibitishwa na Seneti. Vivyo hivyo kwa Mahakama ya Rufaa, nao wanateuliwa na rais aliyepo madarakani.

Leo kwa mfano, kati ya majaji tisa wa Mahakama ya Upeo (Supreme Court), majaji 6 waliteuliwa na marais wa Chama cha Republican na watatu waliteuliwa na marais wa Chama cha Democrat. Kwa Marekani, Jaji wa Mahakama ya Upeo, Rufaa au Mahakama Kuu, hastaafu. Wanaondoka madarakani wanapofariki dunia au kwa kujiuzulu.

Sitanii katika Mahakama ya Rufaa kati ya majaji 179 wa sasa, majaji 90 wameteuliwa na marais wa Chama cha Republican na majaji 89 wameteuliwa na marais wa Chama cha Democrat. Hii ina maana kesi inapofika mbele ya mahakama, inaangaliwa kwa jicho la kisiasa kwanza, iwapo wewe ni mfuasi wa Chama cha Democrat au Republican na ndipo unatendewa haki kwa mujibu wa sheria!

Jaji Juan Merchan wa Mahakama ya Rufaa ya Jimbo la New York, anayesikiliza kesi ambayo Wazee wa Baraza wamemtia hatiani Trump kwa makosa 34 Mei 30, 2024, naye ni mwanachama wa Chama cha Democrat. Aliteuliwa na Meya wa New York, Mike Bloomberg M-Democrat, mwaka 2006. Kama nilivyosema, hata mahakama za rufaa za majimbo majaji wake wanateuliwa na viongozi wa kisiasa, ambao kwa ngazi ya majimbo mteuaji ni meya.

Sitanii, mahakama za rufaa za majimbo yote 50 ya Marekani, hukumu zake zinapingwa katika Mahakama Kuu ya Shirikisho, Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho na Mahakama ya Upeo ya Shirikisho, ambayo wengine wanaiita Mahakama ya Juu.

Kwa maana hiyo, Trump kutiwa hatiani katika Mahakama ya New York, inayofahamika kama Manhattan, haimaanishi huo ndio ulikuwa mwisho wa reli. Alikuwa na nafasi ya kukata rufaa kwenye mahakama za shirikisho.

Pamoja na kwamba Jaji Merchan ni mwanachama wa Democrat, baada ya wazee wa Baraza kumtia Trump hatiani Mei 30, 2024 busara ilimwingia. Jaji Merchan, alikataa kutoa hukumu mwezi Oktoba. Ikumbukwe katika mashitaka kuna kupatikana na hatia na kuhukumiwa. Hakutoa hukumu kutokana na masuala mawili; moja, kampeni za urais kati ya Trump na Harris Kamala zilikuwa katika hatua za mwisho. Lakini la pili, ni hukumu ya Mahakama ya Juu ya Julai 1, 2024.

U.S. Republican presidential candidate businessman Donald Trump speaks at a veteran’s rally in Des Moines, Iowa January 28, 2016. REUTERS/Aaron P. Bernstein

Katika msururu wa kesi, Trump alikuwa amekata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya Jimbo la Colombia, ambayo majaji watatu – Florence Pan, Karen L. Henderson na J. Michelle Childs, walikuwa wametupilia mbali rufaa ya Trump juu ya mipaka ya Kinga ya Rais wa Marekani. Hii ilitokana na Trump kumwelekeza Makamu wa Rais (wakati huo) Mike Pence, akahakiki iwapo Biden alipata ushindi kihalali.

Trump alishitakiwa kwa maelekezo haya. Katika kesi hii alikuwa akijenga hoja kuwa maelekezo aliyoyatoa, aliyatoa kwa mamlaka yake kama Rais wa Marekani na si kama mtu binafsi. Februari 6, 2024 majaji hao watatu katika Mahakama ya Rufaa ya Jimbo la Columbia walitupilia mbali rufaa ya Trump.

Trump katika kesi ya Manhattan alikuwa anasema baadhi ya mambo anayoshitakiwa nayo katika makosa 34, baadhi yanaangukia chini ya Kinga ya Urais wa Marekani, kwani Rais wa Marekani katiba inasema asishitakiwe kwa jambo lolote, iwe la jinai au madai alilolitenda akiwa madarakani.

Julai 1, 2024 kwa utaratibu ule ule nilioutaja hapo juu, baada ya Trump kuwa amekata rufaa kwenye Mahakama ya Juu/Upeo ya Marekani yenye majaji 9 wa kudumu, ambao kuondoka kwao ni lazima afe au ajiuzulu na kati yao majaji sita ni wanachama wa Chama cha Republican na watatu ni wanachama wa Chama cha Democrat, walitengua hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya Jimbo la Colombia kwa uamuzi wa kura 6/3, uliompa ushindi Trump.

Sitanii, hukumu hiyo ya Julai 1, 2024 inatengua baadhi ya hatia alizotiwa Trump katika makosa 34 ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya Manhattan, New York. Ni katika msingi huo nimesema Jaji Merchan, mbali na kubaini kuwa amefungwa mikono, busara ilimwingia akasema hatoi hukumu hadi uchaguzi ukamilike, kwa maana kuwa ataitoa Novemba 26, 2024.

Kwa mujibu wa sheria za Marekani, Trump alipaswa kufungwa gerezani au kifungo cha nje kutokana na kutiwa hatiani kwa makosa 34, lakini kama nilivyosema hukumu ya Mahakama ya Juu ya Julai 1, 2024, iliyafifisha baadhi ya makosa aliyohukumiwa nayo. Si hilo tu, Trump amechaguliwa tena kuwa Rais wa Marekani akimshinda Kamala Harris kwa kishindo, ambapo amechukua Seneti kwa kupata maseneta 53 hadi sasa, wakati alihitaji 50 tu, na Bunge la Wawakilishi anaelekea kulichukua, kwani tayari anao wabunge 215 kati ya 218 wanaohitajika. Na katika hao, amechukua viti vitano kutoka kwa waliokuwa wabunge wa Democrat.

Sitanii, kichekesho cha sheria za Marekani ni cha aina yake. Mfungwa hazuiliwi kugombea urais. Adhabu pekee anayopata ni kupoteza haki ya kuwa uraiani, kwani kama ni kura anapiga na kupigiwa. Akishinda, Katiba ya Marekani inasema Rais aliyeko madarakani au Rais Mteule, hafungwi gerezani. Hivyo, hata kama wangemhukumu kwenda gerezani, Trump angetumikia kifungo kwa muda mfupi na iwapo angeshinda urais akiwa gerezani, malango yangefunguliwa akatoka.

Nimeandika kwa kina mlolongo wa baadhi ya kesi dhidi ya Trump kwa nia ya kuonyesha siasa zinavyotumika vibaya. Mwanasheria Mkuu wa Marekani, tayari mwezi huu ameanzisha mchakato wa kufuta kesi zote dhidi ya Trump zilizoko mahakamani. Mara kadhaa, Rais Joe Biden alidhani Trump kwa kufunguliwa kesi hizo wananchi wangemchukia. Kumbe, alimpa umaarufu. Trump naye alikuwa kila mara akisema kesi hizo alizofunguliwa ni za kisiasa, na wananchi wakamwelewa.

Wafuasi wa Chama cha Democrat katika mwezi wa Oktoba na Novemba hii, wamemlalamikia mno Jaji Merchan, kwa madai kuwa angetoa hukumu ya kumfunga Trump, wao ingewasaidia. Wanaona baadhi ya wapigakura wangemchukia Trump, hivyo kumnyima kura. Ndiyo maana katika kampeni Harris alikuwa akitamba kuwa yeye kama wakili, ana uzoefu wa kufunga wahalifu kama Trump, hivyo wamchague akina Trump waozee magerezani.

Kwa hizi kesi nyingi alizofunguliwa, mimi ni mmoja wa watu waliokuwa wanamchukia Trump kutokana na kauli yake ya kutuita Afrika kuwa ni sawa na ‘Shimo la choo’, lakini hadi mwezi Machi, mwaka huu, nilikwisha kuanza kuwa mfuasi wa Trump. Nampenda. Yapo mambo yaliyonifanya nimpende Trump. Jambo la kwanza, Trump hapendi vita. Ameapa kumaliza vita kati ya Ukraine na Urusi, iliyoua uchumi wa dunia.

Kwa ufupi, Urusi ilikuwa inazalisha mapipa milioni 12 ya mafuta ghafi kila siku. Joe Biden na washirika wake wameiwekea Urusi vikwazo, bei za mafuta zimepanda kuliko maelezo duniani, ikiwamo kwao Marekani na hapa Tanzania. Kwa Trump kuapa kumaliza vita hii, atanusuru uchumi wa dunia, ambao Marekani inauangusha bila kujua.

Jambo la pili ambalo leo nawekea ukomo, ni suala la Trump kupinga ushoga. Joe Biden na washirika wake walikuwa wanataka kila nchi itunge sheria ya kuruhusu wanaume kuolewa. Uganda wameiwekea vikwazo kwa Rais Yoweri Museveni kutunga sheria inayozuia ushoga. Trump amesema mchezo wa vijana wa kiume kujigeuza jinsia na kuwa wa kike, usagaji na ushoga, anapoingia madarakani anavipiga marufuku mara moja.

Nchi zetu zinahitaji barabara, maji, elimu, huduma za afya na mambo mengine mengi. Marekani haitupatii hata mkopo wa dola bilioni 10, Biden na washirika wake wanatoa mkopo wa dola bilioni 5 kwa nchi 54 za Afrika katika kipindi cha miaka 5, lakini wametoa dola bilioni 80 kwa Ukraine inunue mabomu ya kuipiga urusi! Vijana wamekufa wamekwisha Ukraine, sasa wameshusha umri wa kulazimisha watu kwenda jeshini kutoka miaka 27 hadi 25. Ukisikia wanachotafuta ni ujinga eti Ukraine ijiunge NATO wapate nafasi ya kupambana na Urusi!

Sitanii, makala hii imekuwa ndefu. Ushindi wa Trump ni ushindi dhidi ya maovu na kurejea kwa uchumi bora na imara duniani.

Amani ikitamalaki duniani, ni wazi tutafanya biashara, hatutakuwa na vita na hali zetu kiuchumi zitaimarika. Kwa msingi huo, ninasema bora Trump anayetutukana bila kutuhujumu kuliko Kamala aliyekuwa ameapa kuendelea kutulazimisha ushoga. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827