Rais Donald Trump ameweka saini agizo linalotangaza Kiingereza kuwa lugha rasmi ya Marekani, hatua inayobatilisha sera ya awali iliyoanzishwa na Rais Bill Clinton mwaka 2000. Sera hiyo ilihitaji mashirika ya serikali kutoa msaada kwa watu wasiozungumza Kiingereza.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Marekani, tangu kuanzishwa kwake karibu miaka 250 iliyopita, kwa nchi hiyo kutaja rasmi lugha moja kama lugha rasmi ya shirikisho.

Kwa mujibu wa amri hiyo, mashirika ya serikali hayahitajiki kubadili, kuondoa, au kusitisha huduma yoyote ya lugha ambayo tayari wanatoa. Hii inamaanisha kuwa msaada wa lugha kwa wasiozungumza Kiingereza utaendelea kama ilivyokuwa awali.

Licha ya hatua hii, takwimu kutoka Ofisi ya Sensa ya Marekani zinaonyesha kuwa takriban milioni 68 kati ya milioni 340 za wakazi wa Marekani wanazungumza lugha nyingine zaidi ya Kiingereza. Lugha hizi ni pamoja na zaidi ya lugha 160 za Wenyeji wa Marekani.

Kihispania, Kichina, na Kiarabu ni baadhi ya lugha zinazozungumzwa na idadi kubwa ya watu nchini Marekani, baada ya Kiingereza. Ingawa hatua hii ilijaribiwa na chama cha Republican miaka ya nyuma, juhudi zao za kutengeneza sheria ya lugha rasmi ya Marekani zilishindwa mwaka 2021. Wapinzani walieleza kuwa lugha rasmi haina haja ya kuwa lugha inayozungumzwa na idadi kubwa ya watu, na kwamba kuifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi kunaweza kuleta ubaguzi dhidi ya wale wasiozungumza Kiingereza.

Katika ulimwengu, nchi karibu 180 zina lugha rasmi za kitaifa, ambapo nchi nyingi hutambua lugha rasmi zaidi ya moja. Hata hivyo, baadhi ya nchi, kama vile Uingereza, hazina lugha rasmi.