Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema atafanya mazungumzo na viongozi wa Ukraine na Urusi kumaliza alichokitaja kuwa “umwagaji damu usiomithilika” kutokana na vita vya karibu miaka mitatu baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi habari tangu alipochaguliwa kwa mara nyingine kuwa rais wa Marekani, Trump amesema ni lazima mauaji yanayotakana na vita hivyo yakomeshwe, akiahidi kwa mara nyingine kuumaliza mzozo huo atakapoingia madarakani.
“Tutazungumza na Rais Putin, na tutazungumza na wawakilishi, Zelensky na wawakilihsi wa Ukraine,” amesema Trump kwenye mkutano huo ba waandishi habari uliofanyika kwenye makaazi yake huko Florida.
“Ni lazima tukomeshe (vita), ni mauaji yasiyoelezeka,” amesema kiongozi huyo atakayeapishwa kuchukua hatamu za uongozi mnamo Januari 20 mwaka ujao.
Trump mara kadhaa amedai kuwa na uwezo wa kumaliza mzozo wa Ukraine haraka lakini hadi sasa hajaweka wazi hadharani mkakati wake wa kufanya hivyo.
Hivi karibuni alitoa mwito wa kushitishwa mara moja kwa mapigano na akasema “mazungumzo yanapaswa kuanza haraka.”