Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) limesaini mkataba na sekta binafsi ya kuleta treni ambazo zitabeba mizigo kutoka bandarini na kupeleka nchi jirani.

Mkataba huo umesainiwa Machi 20, 2024 Makao Makuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Bruno Ching’andu na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Usafirishaji Makontena ya Bravo Group Limited, Angelina Ngalula ambaye pia ni Mwenyekiti wa wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Akizungumza Ching’andu amesema makubaliano hayo yanalenga kupanua ukuaji wa uchumi na fursa za biashara ndani ya ukanda wa Dar es Salaam sambamba na kuimarisha biashara ya ndani ya Kanda ya SADC.


“Ushirikiano huu unaonyesha nguvu ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika kutoa huduma,” amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Bravo, Angelina Ngalula ametoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo yanahimiza uwekezaji na ukuaji wa biashara, na kusababisha fursa za ajira na michango chanya katika Pato la Taifa (GDP).

Amesema wamewekeza zaidi ya Sh bilioni 20 kwenye mradi huo ambazo ni kujenga eneo la kuweka mizigo na vifaa mbali mbali.

Ngalula amesema mkataba huo utawawezesha sekta binafsi kuleta treni ambazo zitatoa mzigo bandarini kwenda kwenye nchi zinazotunguzuka za ukanda wa SADC ikiwemo Zambia na Congo.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF Octavian Mshiu amesema Tazara inakuwa kampuni ya kwanza ya reli kushirikisha sekta binafsi kupitia makubaliano yaliyosainiwa leo.

Kwa upande wa Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Rahim Dosa, ameipongeza hatua hiyo na kufafanua kuwa biashara hiyo haitashindana na biashara ya malori. Badala yake, wanaiunga mkono kwa kuwa itaongeza sehemu ya soko la bandari na wingi wa mizigo