TRC: KUSIMAMA KWA TRENI YA MCHONGOKO NI HUJUMA

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limeutaarifu umma kupuuza taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu kuhusu kusimama kwa treni za EMU, Electric Multiple Unit (mchongoko) pamoja na changamoto za umeme, ikisema kuwa haijawahi kuwa na changamoto za umeme.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 6, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala imeeleza kuwa tangu kuanza kwa safari ya kwanza ya treni zinazotumia nishati ya umeme Juni 14, 2024 hakujawahi kuwa na changamoto ya umeme.

“Tunawashukuru wenzetu wa TANESCO kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa. Aidha, kilichotokea Novemba 3, 2024 na kusababisha kusimama kwa treni ya EMU kwa takribani saa 6 ni hujuma kutokana na kukatika ama kukatwa kwa nyaya (catenary) zinazochukua umeme kutoka njia ya umeme kupeleka kwenye treni.

“Shirika la Reli Tanzania linauhakikishia umma kuwa hakuna treni ya Mchongoko iliyopata hitilafu ya kiufundi.

Tayari baadhi ya wahusika wamekamatwa na hatua stahiki dhidi yao zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo

kufikishwa kwenye vyombo husika,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha Shirika hilo limewakumbusha wananchi kuwa bado tuko kwenye kipindi cha mwaka mmoja cha matazamio, na kama changamoto zozote zinajitokeza, TRC itaujulisha umma kwa uwazi kama siku zote tunavyofanya, na taarifa rasmi mtazipata kwenye vyanzo vyetu rasmi na si vinginevyo.

“TRC inawashukuru abiria kwa uvumilivu kipindi cha changamoto,” imeongeza taarifa hiyo.