Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Soga

Shirika la Reli la Tanzania (TRC) limeingia makubaliano ya kibiashara na Shirika la Reli la Korea Kusini (Korail) yatakayoimarisha ushirikiano katika kuendeleza miundombinu ya reli barani Afrika.

Makubaliano kati ya mashirika haya mawili yanaingia katika historia kwa kuwa ni ya kwanza ya aina yake kufanyika ndani ya treni ya kisasa (SGR) wakati wa safari yake ya kwanza rasmi kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma, yakisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, na Rais wa Korais, Han Moon-hee, kwa niaba ya serikali ya Korea.

SGR inatarajiwa kuiunganisha Tanzania na mataifa ya Rwanda, Burundi, Uganda na Sudan Kusini; ambapo Korail imedhamiria kuwa mshirika mkubwa katika mradi huo barani Afrika.

Chini ya makubaliano, Korail itaisaidia TRC katika masuala ya uendesha wa reli pamoja, utaalamu na teknolojia ya kiufundi, huku TRC ikiahidi kusapoti masuala ya utawala kwenye miradi ya Korail nchini.

Hayo yote yamewezekana kufuatia mkutano kati ya viongozi hao wakuu wa mashirika ya reli ya Tanzania na Korea; Han na Kadogosa, wakati wa mkutano wa kilele wa ushirikiano kati ya Korea na Afrika (Korea-Africa Summit) uliofanyika jijini Seoul, Korea Kusini, Juni mwaka huu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi ndani ya treni ya SGR, Han amesema ndani ya makubaliano kuna mradi wa uendeshaji na ukarabati (O&M) wa (SGR).

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa (kulia) na Rais wa Shirika la Reli la Korea (Korail), Han Moon-hee, wakipeana mikono baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara (MoU) kati ya mashirika hayo. Hafla hiyo ilifanyika ndani ya treni ya SGR iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma wiki iliyopita.

“Mradi huu unahusisha ushiriki wa moja kwa moja wa Korail katika uendeshaji wa treni na ukarabati wa jumla wa mabehewa na maeneo mengine katika reli ya kati kipande cha kilomita 450 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Mkataba huu utakamilishwa mwishoni mwa mwaka,” amesema Han.

Han pia amepnyesha nia ya Korail kushiriki katika maendeleo ya uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya reli ya zamani (MGR) na kukiboresha Chuo cha Reli.

Kwa upande wake, Kadogosa amezungumzia uwezo mkubwa wa kiteknolojia walionao Korail, ambao umekuwa ukionyeshwa tangu mwaka 2014 kupitia upembuzi unaofanywa katika reli ya kusini mwa Tanzania (Mtwara Line), huduma ya ushauri katika ujenzi wa SGR, akiweka wazi kuwa:
“Korail ni mshirika muhimu wa miradi ya reli ya Tanzania. Tuna mengi ya kujifunza kwao na tunaahidi kuiga yote mazuri waliyonayo.

“Ni safari ya Korea ya Rais Samia Suluhu Hassan ndio imezaa hii ‘MoU’. Tunaishuru sana Korea Kusini kwa kuwa mshauri kwenye miradi yetu mingi.

“Mabehewa, injini vyote vimenunuliwa kutoka Korea… Hata madereva kwa sasa ni waKorea. Kwa nini Korea? Hawa ni namba tano katika mashirika bora ya reli duniani. Tumejifunza huko kwamba ‘punctuality’ (uzingatiaji wa muda) ya treni za Korea ni asilimia 100. Na sisi tunaiga hali hiyo, kuhakikisha kuwa tunachokisema ndicho hicho.

“Ajali Korea ni zero. Ushirikiano huu utakuwa ni wa manufaa makubwa kwa Watanzania wote na utaifanya TRC kuendesha treni na shirika kwa weledi wa hali ya juu.”

Please follow and like us:
Pin Share