Wanachama wa matawi matano wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU) wamekutana jijini Dar es Salaam na kuunga mkono uamuzi wa Kamati Maalumu ya Dharura wa kuwasimamisha kazi viongozi wa kitaifa wa chama hicho.

Hatua hii imetokana na mgogoro ulioanza baada ya uongozi wa TRAWU kupindua mapendekezo ya wanachama siku ya Mei Mosi, 2019, ambapo mtumishi waliyemchagua awe mfanyakazi bora, viongozi walifanya mchezo mchafu akapewa ufanyakazi hodari na mmoja wa viongozi akateuliwa kuwa mfanyakazi bora badala yake.

Bona Mwengele amesema pamoja na viongozi hao kumdanganya rais kwa kumpelekea jina la mfanyakazi bora ambalo halikupendelezwa na wafanyakazi, bado wanaamini kuwa mfanyakazi bora ni yule waliyempendekeza na si vinginevyo.

Ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wake wanadaiwa kuwasilisha jina la kigogo asiyestahili kuwa mfanyakazi bora, akapewa mkono na Rais Dk. John Magufuli na kukabidhiwa cheti cha mfanyakazi bora na zawadi ya hundi.

Katika mchakato wa kumsaka mfanyakazi bora kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania kinachohusisha pande mbili; wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na wale wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), mambo yalikwenda vizuri, lakini matokeo yaligeuzwa dakika za mwisho wakati shughuli za kilele cha Mei Mosi zikiendelea Uwanja wa Sokoine, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.

Katika mchakato wa upigaji kura, JAMHURI limethibitishiwa kuwa mfanyakazi wa kada ya chini, James Kunena, ndiye aliyeshinda kuwa mfanyakazi BORA kwa mujibu wa kura zilizopigwa kupitia TRAWU.

Hata hivyo, kutokana na hila zilizofanywa na baadhi ya viongozi, walifanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi HODARI, kwa hiyo kulikuwa na mshindi wa kundi la mfanyakazi BORA ambaye ndiye anastahili kuhudhuria sherehe za kitaifa za Mei Mosi na kukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi.

“Mshindi wa tuzo ya mfanyakazi BORA TRAWU kwa mujibu wa kura za wafanyakazi ni James Kunena, na mshindi wa tuzo ya mfanyakazi HODARI ni Focus Sahani, ambaye ushindi wake ulipatikana baada ya kura kupigwa kwa raundi tatu.

“Wafanyakazi wote tulijua kwamba Kunena ndiye mshindi wetu, na atakuwa katika sherehe za kitaifa Mbeya kukabidhiwa zawadi zake, jambo ambalo lingetupatia hamasa zaidi sisi wafanyakazi wa kawaida, lakini kinyume chake, akatangazwa Focus Sahani ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji TRL,” ameeleza mmoja wa watoa habari wetu hivi karibuni.

Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TRAWU unatarajiwa kufanyika Septemba 5, jijini Dodoma huku ajenda kuu ikiwa ni nafasi ya viongozi walioondolewa madarakani na kuiomba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mfuko wa chama hicho.

Katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki Msimbazi Centre, Dar es Salaam wanachama hao ambao ni viongozi wa matawi ya TRAWU kanda za TRC na TAZARA walieleza kuwa hawako tayari kuendelea kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Ole Saitabau na Katibu wake, Nashon Malyeri.

Akizungumza katika mkutano huo, David Kayange, amesema tangu viongozi hao washike madaraka hawajawahi kuitisha mkutano na wanachama kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi, bali wamekuwa wakishiriki kwenye vikao vya utawala, ambapo hulipwa posho ya dola 100 za Marekani kila kikao.

Amesema wameshindwa kuhuisha mkataba wa makubaliano wa pamoja wa TRC, hivyo kusababisha wafanyakazi kuishi maisha duni yasiyoendana na mabadiliko ya kimaisha kutokana na mkataba wao kuwa nyuma kwa miaka minane.

Kayange amesema: “Mfanyakazi wa TRC anapostaafu barua yake haielezi wazi stahiki zake, lakini pia hata posho zinazolipwa sasa ni hesabu za miaka zaidi ya saba, kwani tunalipwa Sh 30,000 tu ambayo inaitwa posho maalumu.”

Amesema kwamba kwa umoja wao wanaunga mkono hatua ya kikao cha Agosti 9-10, mwaka huu kwani ni hatua nzuri ya kumkomboa mfanyakazi wa reli nchini.

“Tunaomba ieleweke kwamba uanzishwaji wa vyama vya wafanyakazi nchini ni kwa ajili ya kulinda ajira pamoja na kutetea hali na masilahi ya wafanyakazi. Bila TRAWU imara hakuna TRC/TAZARA, haki ni lazima zilindwe kwa kuzingatia misingi ya sheria na kanuni za nchi,” amesema.

Viongozi hao wameeleza masikitiko yao kwa uongozi uliosimamishwa kuwa wamekuwa wakiwachonganisha na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwasingizia kuwa wanahujumu mradi wa SGR.

“Hivi karibuni tulipokuwa kwa msajili nimesikia mambo yanayoumiza, wamekwenda kule wanaanza kusema sisi wafanyakazi tunahujumu ujenzi wa reli unaofanywa na mheshimiwa rais, jambo ambalo si kweli, kwani tunashukuru sasa tutakuwa kama nchi za wenzetu,” amesema mmoja wa wajumbe.

Imeelezwa kuwa viongozi waliosimamishwa walikutana na uongozi wa TRC na kuueleza kuwa wanachama wa TRAWU wamekuwa wakitumiwa na vyama vya upinzani hasa CUF. Pia kwamba wafanyakazi wa TAZARA wamekuwa wakiihujumu TRC, jambo ambalo si kweli.

Wamesema kutokana na hali ilivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alipotembelea TAZARA alisema wazi kuwa chama cha wafanyakazi kimenunuliwa na wafanyakazi hawana mtetezi.

Wamesema kwamba wanaamini juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kufufua njia ya reli ya Tanga kwenda Moshi na kuifanya reli hiyo kuwa ya kisasa, si jambo la kubezwa na Mtanzania yeyote mpenda maendeleo.

Beatus Mwakimbwala ameeleza kuwa viongozi walioondolewa kazini wamekuwa wakikihujumu chama na wanachama, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuwashambulia viongozi wa matawi na kanda kuwadhoofisha wanachama.

Mwakimbwala ameeleza kuwa wamekuwa wakiwachonganisha baadhi ya wafanyakazi na utawala kwa kuhariri barua huku akitoa mfano wa barua ya Juni 26, mwaka huu kwenda kwa Kamati Kuu ambayo Ole Saitabau aliihariri na kuipeleka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TRC kwa nia ya kuwachonganisha.

“Tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli kwa kuanzisha ujenzi wa reli ya kisasa kwa fedha za ndani, kazi yetu sisi ni kuhakikisha tunafanya kazi kwa juhudi na maarifa huku mwajiri wetu akizingatia misingi ya sheria na kuimarisha mashirika yetu mawili ya TRC na TAZARA,” amesema.