Jumanne, Machi 20, 2018 ni siku ambayo hatuwezi kuisahau sisi waongoza watalii watatu.
Tulifanyiwa kitendo cha uonevu wa hali ya juu pamoja na kunyanyaswa wageni watalii, raia wa
Marekani tuliokuwa tukiwapeleka Sirari.
Tukio hili tulifanyiwa na polisi trafiki katika wilaya za Rorya na Tarime mkoani Mara.
Tulibambikiwa makosa, tukalipishwa faini na kuwachelewesha wageni, hali iliyowafanya
wakasirike sana.
Tulikuwa na msafara wa magari matatu tukiwasafirisha kwenda Sirari. Njiani tulikuta kizuizi cha
polisi ambao walituruhusu kuendelea. Baada ya kupita walitupiga picha kwa nyuma na kurusha
kwa wenzao mbele ambao walitusimamisha na kudai eti kwenye kizuizi cha kwanza tulizidisha
spidi. Mimi nikawa eti na spidi 46 badala ya 30 na mwenzangu akawa na 42 badala ya 30.
Hii si kweli kwa sababu mahali hapo hapakuwa na alama yoyote na ndiyo maana tulipofika
kwenye kizuizi kulikuwa kumeandikwa 30/km na tulitii, tukasimama na kuruhusiwa kuondoka.
Lakini mbele askari wakadai tulipe faini Sh 30,000 sisi wawili. Tukabishana sana na tuliomba
waturuhusu tukawaache wageni kisha tungerudi tukaone kwenye tukio. Walituruhusu ila papo
hapo wakarusha taarifa mbele zaidi eti tumekimbia amri ya polisi!
Basi hao tukawaomba waturuhusu tungerudi tu na kwamba tumeshawachelewesha wageni.
Tulikuwa na mgeni mwingine mgonjwa wa kisukari, hivyo alihitaji kutumia maliwato mara kwa
mara.
Tukaendelea na tulipofika mpakani Sirari, dada mmoja Afisa Uhamiaji alipata hizi habari na
kumtafuta RCO wa Tarime. RCO alitutaka tufike kituoni Tarime, tukajieleza kwake, akatuelewa;
hatujawakimbia polisi ila suala la faini turudi kwa wale askari.
Tukarudi hatukuona alama yoyote kuashiria mwendo wa 30/km. Tukalazishwa kulipa faini.
Tukalipa. Sasa cha kustaajabisha yule mwenzetu wa tatu ambaye awali yeye hakuguswa,
tunaondoka pale tulipolipia faini – wakampiga picha kwa nyuma. Picha ikarushwa mbele.
Tukasimamishwa tena. Akawa anatuhumiwa kuwa amezidisha spidi 42/30. Kwanza alitaka
arudi pale kujitetea, lakini asingewezashinda. Pia kama angeamua kurudi nyuma alikopigwa
picha ni kama kilomita 14. Kwa hiyo akalipa.
Namba za magari yetu ni T 487 AWV, T 482 AWV na T 235 BFJ. Tunaomba mamlaka
zinazohusika zitusaidie kuchunguza uonevu huu kwani ni kero sana kwetu na kwa watalii.
Trafiki wanajificha na kupiga picha katika maeneo ambayo hata hakuna alama ya kuonesha
mwendo unaotakiwa. Wanachofanya ni kupiga picha na kisha kukuambia dereva kuwa
umezidisha spidi.
Hali hii inachafua sifa nzuri ya nchi yetu kwa sababu watalii hawa ambao ni Wamarekani
walisema watafikisha malalamiko yao kwenye ubalozi wetu Washington.
Kama kweli tumeamua kubadilika, basi tuunge mkono juhudi za Serikali za kuondoa usumbufu
na rushwa kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu askari hawa waonevu.