Ukisimamishwa na trafiki barabarani na ukawa hauna leseni mfukoni kwa muda huo si kosa. Mwambie huyo trafiki kuwa hilo si kosa. Sheria inataka kutembea na leseni tunapoendesha vyombo vya moto, lakini pia haisemi kuwa utakapokuwa hauna pale unapoombwa na trafiki ni kosa.
Tunazungumzia Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168. Wapo watu wameandikiwa faini kisa wameombwa leseni wakasema hawana, au wakasema wamezisahau majumbani.
Hawa waliotozwa faini katika mazingira kama haya wameonewa. Na wanastahili kurudishiwa fedha walizotoa haraka.
Ni kweli Kifungu cha 77 cha Sheria ya Usalama Barabarani kinamtaka kila mwendesha chombo cha moto kutembea na leseni barabarani. Ni kweli askari anayo mamlaka kumsimamisha mwendesha chombo cha moto.
Na ni kweli pia kuwa askari ana mamlaka ya kumtaka mwendesha chombo cha moto aonyeshe leseni yake. Lakini si kweli hata kidogo kuwa mwendesha chombo cha moto asipoonyesha leseni kwa wakati huo basi tayari ametenda kosa, si kweli.
Kifungu cha 77(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani kinasema kuwa mtu hatatiwa hatiani, kwa maana ya kulipa faini au kuandikiwa kosa au kuadhibiwa na chombo chochote ikiwamo mahakama, kwa sababu tu hakubeba, au hakutoa/kuonyesha leseni pale alipotakiwa kufanya hivyo, isipokuwa ana siku tatu za kutoa au kuonyesha leseni hiyo tangu siku hiyo aliposimamishwa.
Iko wazi kuwa unaposimamishwa, ukaombwa kuonyesha leseni, ukawa hauna kwa muda huo, unazo siku tatu mbele za kutakiwa kuleta na kuonyesha. Anachotakiwa kufanya askari si kukuandikia kosa, bali ni kukutaka umuonyeshe leseni hiyo ndani ya siku tatu tangu siku hiyo. Ukishindwa kufanya hivyo ndani ya siku hizo hapo ndipo linaweza kuwa kosa.
Watu wasionewe, wapo askari wengine pia hawajui hizi sheria. Madereva tuwaelimishe askari, unaweza kudhani askari anakuonea kumbe naye hajui.
Kwa hiyo kazi unayo wewe kuhakikisha unamweleza huyo askari kuhusu kifungu hiki na namna kinavyotaka. Wewe ndiye mtetezi wa kwanza wa haki yako kabla ya kutetewa na mtu mwingine.
Na kama ikitokea umeandikiwa adhabu kwa lazima kwa kitu kama hiki, basi unayo haki ya kukataa kulipa na kuomba kufikishwa mahakamani ili sheria ikatafsiriwe.
Mwambie: “Sitalipa, nataka sheria ikatafsiriwe mahakamani.” Kukataa kulipa si kosa au ukorofi, hivyo hauna haja ya kuhofu. Kukataa kulipa ni haki katika haki ulizonazo ukihisi umeonewa.
Na kama umeshalipa au ulilipa huko nyuma katika mazingira ya jambo kama hili na unao ushahidi, basi unayo haki ya kudai fedha ulizolipa. Unaweza kuzidai huko ulikotozwa au mahakamani.
Sheria imetoa ahueni hii ikizingatia mazingira ya ubinadamu. Hauwezi kila unapoamka asubuhi ukakumbuka leseni. Hauwezi kila unapokuwa na safari ukakumbuka leseni.
Safari nyingine ni za ghafla na za kushtua, mfano kuitiwa msiba, ugonjwa, matatizo kazini, bila kusahau msongo/stress za ada na kodi. Atapata wapi muda wa kukumbuka leseni mtu huyu?
Mwingine amebadilisha nguo, hivyo leseni kubaki kwenye nguo iliyovuliwa. Mwingine amebadilisha gari, hivyo leseni kubaki kwenye gari jingine. Na mazingira mengine kama hayo. Zote hizi ni dharura za kibinadamu zilizowafanya watunga sheria kuweka muda wa siku tatu kwa ajili ya kutoa au kuonyesha leseni.
Basi wote tubadilike, madereva na askari wasimamia usalama barabarani. Dereva asiwe mkorofi, kadhalika askari asimwonee dereva.