Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewaasa wananchi wanaotembelea maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) waweze kufika katika banda lao ili waweze kupata elimu kuhusiana na masuala ya kodi pamoja na shughuli mbalimbali wanazofanya.

Hayo yameelezwa na Afisa Mwandamizi wa Kodi kutoka Mamlaka hiyo, Philipo Eliamini wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema maonesho hayo yanawapa fursa kuonana na wananchi kuwapa elimu mbalimbali ikiwemo ya masuala ya kikodi na usimamizi wa kodi pamoja na kupokea maoni na malalamiko ya wananchi ambayo pia kuwawezesha kuboresha utendaji wao wa kila siku.

“Kama mnavyofahamu wadau wa maonesho haya ni wakulima na Wafugaji na tunasema kilimo ni biashara, lakini tunafahamu serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye masuala ya kilimo na inatoa misamaha mbalimbali kwenye eneo la kilimo ambapo matarajio ni kwamba wakulima hawa wanapofanya shuguli hizo na kupata kipato kitakachofikia kiwango cha kutozwa kodi basi na wao waweze kuichangia serikali katika masuala mazima ya kodi.

“Kwa hiyo tunasema maonesho haya ni fursa nzuri kwa wananchi kujifunza lakini pia ni fursa nzuri kwetu ambapo tunaweza kuonana na wadau wetu na tunawapa elimu ambayo itawasaidia katika shughuli zao,”amesema.

Amefafanua kuwa, kila mwaka serikali kupitia Bunge inafanya mabadiliko ya Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria za kodi na kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 kumefanyika mabadiliko mbalimbali ya kikodi ambapo, kwa upande wa sheria za kodi kuna misamaha mbalimbali ya kodi ambayo italeta unafuu mkubwa kwa wakulima.

Ameseongeza kuwa, wanayatumia maonesho hayo kutoa namba ya utambulisho wa mlipa kodi kufuatia mabadiliko ya sheria ya mwaka jana ambayo yaliweka kipengele cha kila raia kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea anapaswa kuwa na namba hiyo ya utambulisho wa mlipa kodi ambapo muhusika anapaswa kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Amesema pia wanatoa huduma ya makadirio ya kodi kwa mfanyabiashara ambaye bado hajakadiriwa makadirio ya kodi kwa mwaka huu wa fedha lakini pia kwa wanaodaiwa kodi na wanahitaji kupata namba za malipo huduma hiyo inapatikana.

“Wasambazaji wa mashine za kutolea risiti za EFD na zile za VFD, wanatoa elimu ya matumizi ya mashine hizo na wataalam wapo, na mashine zipo kwa wanaohitaji kununua ,ambapo kila mfanyabiashara mwenye mauzo ya kuanzia Shilingi Milioni 11 kwa mwaka anapaswa kununua na kutumia mashine hizo,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share