Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imevipongeza vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari nchini, kwa kuhamasisha wananchi hasa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari,kujua umuhimu wa kudai risti wanaponunua bidhaa na wafanyabishara kutoa risti wanapouza bidhaa.

TRA imesema,hatua hiyo imewezesha Mamlaka kuvuka lengo kwa kukusanya kiasi cha Sh.trilioni 7.53 kati ya Mwezi Januari hadi Machi 2025 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 13.47 ukilinganisha na kiasi cha Sh.trilioni 6.63 zilizokusanywa katika kipindi cha kama hicho kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka hiyo Richard Kayombo wakati akitoa salamu za Kamishina Mkuu wa TRA Tanzania kwenye Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF) wa kuchagua viongozi wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa Parokia ya Bombambali Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa Kodi TRA Richard Kayombo akizungumza kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa TEF mkoani Ruvuma.

Aidha alisema,Makusanyo yaliyokusanywa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025 yanapelekea TRA kuweka rekodi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kufikiwa na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 9 mfululizo tangu kuanzishwa kwake.

Kwa mujibu wa Kayombo, ni kwamba,sehemu kubwa ya mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa uliofanywa na wanahabari na wahariri wa vyombo vya habari, ambao wamekuwa wakitumika kama daraja la kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Kayombo alisema kwamba mafanikio haya yanatokana na ushirikiano mkubwa kati ya TRA na wahariri, ambapo wamekuwa wakishirikiana na TRA pale panapotokea changamoto au maswali, kwa kutoa ufafanuzi au taarifa muhimu kwa jamii.

Aliongeza kuwa mafanikio haya yamewezesha TRA kuongeza wigo wa ushirikiano na vyombo vya habari, hivyo kufanikisha malengo ya ukusanyaji mapato kwa miezi tisa mfululizo.

Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile akiwashukuru wajumbe mara baada ya uchaguzi.

“TRA inajivunia mafanikio haya ambayo yameletwa na juhudi za pamoja, Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali, vyombo vya habari, na jamii, Hatua hii pia inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miundombinu ya usafiri, hasa barabara na njia za usafiri wa hanga ambazo awali zilikuwa hazipo,” alisema Kayombo.

Katika mkutano huo, Kayombo pia aliwashukuru wahariri kwa mchango wao mkubwa katika kuchochea umoja baina ya walipa kodi na TRA, na aliwaomba kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti, ili kuhakikisha kuwa malengo ya ukusanyaji mapato yanaendelea kufikiwa.

“Huu ni mfano mwingine wa ushirikiano wa kipekee kati ya vyombo vya habari na serikali, ambao umezaa matunda ya mafanikio ya kiuchumi, na inaonekana kama njia ya kuhakikisha kuwa malengo ya ukusanyaji mapato yanafikiwa kwa manufaa ya wote.”alisema Kayombo.

Kwa upande Afisa Uhusiano Mkuu kutoka TRA, Rachel Nkundai, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kulipa kodi, kwani ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha maendeleo endelevu kwa taifa. Alipongeza wahariri kwa juhudi zao za kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya kodi, na aliwahakikishia kuwa TRA itaendelea kushirikiana nao ili kuboresha sekta ya kodi nchini.

Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma, Nicodemus Mwakilembe, alitoa pongezi kwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kuendesha uchaguzi kwa uhuru na haki. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha umoja ndani ya jukwaa hilo ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana.

Mkutano huu maalumu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania uliofanyika Ruvuma, unatarajiwa kuchochea ongezeko la mapato kwa mwezi ujao, huku Kayombo akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushirikiana na TRA na kudai risiti ili kuchangia maendeleo ya mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla.