Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2019/2020 itahakikisha inaongeza makusanyo ya kodi ili kuiwezesha serikali kutekeleza Dira yake ya Maendeleo ya Taifa kwa kutegemea mapato yake ya ndani.

Akiainisha mikakati watakayoitumia kufanikisha azima hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi, Richard Kayombo, anasema wanatarajia kutumia mifumo ya teknolojia itakayowasaidia kuwafikia walipa kodi wengi kwa urahisi.

Anasema mifumo hiyo ya kiteknolojia itasaidia kupunguza changamoto ya umbali na upotezaji wa muda ambao umekuwa ukisababisha mamlaka hiyo kutokusanya kodi stahiki kwa wakati.

Anaongeza kuwa wamejiandaa kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa walipa kodi kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata, tarafa, wilaya hadi ngazi ya taifa.

“Mpango huo wa kutoa elimu kwa walipa kodi utakwenda sambamba na kuwasajili wateja wapya ambao hawajafikiwa na mamlaka,” anasema.

Aidha, anasema watahakikisha walipa kodi ambao hawajanunua mashine za kielektroniki za EFDs wanazinunua na wanasajiliwa kwenye mfumo wa TRA wa ukusanyaji wa mapato.

“Kumekuwapo malalamiko mbalimbali ya viwango vya kodi kukadiriwa kinyume cha bidhaa na mitaji ya walipa kodi wetu. Ili kuondoa changamoto hii tunataka kuandaa mikutano ya mara kwa mara na walipa kodi wetu na tutawasikiliza changamoto zinazowakabili na kutatua kero zao,” anasema Kayombo.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa ambayo wamefikia katika robo ya pili ya mwaka 2019 iliyoisha mwezi Disemba ambapo wamekusanya jumla ya Sh trilioni 1.987, Kayombo anadokeza kuwa zipo changamoto kadhaa walizokutana nazo.

Anazitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na walipa kodi kutolipa kodi zao kwa wakati huku wengine wakifanya udanganyifu kwenye risiti za malipo.

“Watu wanajisahau sana kulipa kodi, bila shaka changamoto hii inasababishwa na ukosefu wa elimu ya ulipaji kodi. Katika kipindi hiki cha pili tutajitahidi kutoa elimu ili tubaini kama wateja wetu hawalipi kodi kwa makusudi,” anasema Kayombo.

Kwa upande mwingine, amewalaumu wanaofanya biashara kwa njia za magendo kuisababishia mamlaka hiyo kushindwa kukusanya mapato ipasavyo.

 “Watu wamekuwa wakifanya biashara kwa njia za panya, huu ni ukiukwaji wa sheria ya kodi. Tutajitahidi kuzibaini biashara hizo na wanaoziendesha tutawapa elimu ya kodi na kuwasajili kwenye mfumo,” anasema.

Ili kuongeza ufanisi wa kukusanya mapato makubwa, Kayombo anabainisha kuwa wanalenga kuongeza kasi ya kukusanya kodi za majengo, kwani kodi hizo zimekuwa zikilipwa dakika za mwisho kila ifikapo mwishoni wa mwaka.

Naye, Edwin Mhede, Kamishna Mkuu wa TRA, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Januari Mosi alisema viwango vya kodi za majengo kwa sasa ni rafiki.

Alivitaja viwango hivyo kwa mwaka kuwa ni Sh 10,000 kwa nyumba ya kawaida, Sh 50,000 kwa kila sakafu ya nyumba ya ghorofa katika majiji, manispaa na halmashauri za miji na Sh 20,000 kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya halmashauri za wilaya.

 “Tumeweka utaratibu mzuri kwa wamiliki wa majengo kuweza kulipa kodi hii kwa njia ya simu za mkononi. Halikadhalika, tunatarajia kuwa na kampeni nchi nzima ya nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha kila mwenye nyumba analipa kodi hii,” anasema Mhede.

Hata hivyo, anatoa wito kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu vya kughushi au kusafirisha risiti za kielektoniki za EFDs waache mara moja tabia hiyo.

“Operesheni tunayoendelea nayo ya kufuatilia matumizi sahihi ya EFDs waliobainika kukiuka matumizi hayo wamepewa mafunzo mazuri na wengi wao wameacha uhalifu huu wa kikodi. Kila mfanyabiashara na mwananchi atambue kuwa ni wajibu wake wa kisheria wa kutoa na kudai risiti kwa kila mauzo na manunuzi,” anasema Mhede.

Aidha, anasema kupitia matumizi ya mifumo shirikishi, ufanisi umeongezeka kila siku huku akionyesha kuwa ufanisi umeongezeka kwa asilimia 22.05 kutoka Disemba 2018 hadi Disemba 2019.

Mhede anasema makusanyo ya kodi katika robo ya pili ya mwaka 2019/2020 kwa mwezi Disemba 2019 ni jumla ya Sh trilioni 1.987, sawa na ufanisi wa asilimia 100.20.

Anaeleza kuwa kiwango hicho kimevuka malengo yaliyokuwa yamewekwa na mamlaka ya kukusanya jumla ya Sh trilioni 1.983 katika mwezi wa Disemba kwaka jana.

Anaongeza kuwa makusanyo hayo yamevunja rekodi waliyoiweka mwezi Septemba 2019 ambapo TRA ilikusanya Sh trilioni 1.767, sawa na asilimia 97.20 ya lengo lake la kukusanya Sh trilioni 1.817.

Anadokeza kuwa kwa robo ya pili ya mwaka 2019/20 inayohusisha miezi ya Oktoba, Novemba na Disemba, TRA imefanikiwa kukusanya mapato ya serikali jumla ya Sh trilioni 4.972, sawa na asilimia 97.49 ya lengo la kukusanya jumla ya Sh trilioni 5.100 katika kipindi hicho.

Halikadhalika, anasema mafanikio hayo ni kiashiria cha wazi kwa Watanzania, hasa walipa kodi, kwamba wameelewa, kukubali na kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya taifa.