Magari tisa na pikipiki saba yaliyokamatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro yakisafirisha bidhaa za magendo kati ya Tanzania na Kenya yatauzwa kwa njia ya mnada baada ya serikali kuyataifisha.

Miongoni mwa magari hayo limo linalodaiwa kumilikiwa na ofisa mstaafu wa Jeshi la Polisi nchini lenye namba za usajli T 890 CGT aina ya Toyota Mark X.

Magari hayo pamoja na pikipiki yalikamatwa kwa nyakati tofauti katika doria zilizofanywa na maofisa wa TRA kwa kushirikiana na vyombo vya dola  na baada ya wamiliki wake kushindwa kujitokeza, serikali imeyataifisha na wakati wowote yatauzwa kwa njia ya mnada.

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, Meneja Msaidizi Idara ya Forodha, Edwin Iwato, amesema vyombo hivyo vya usafiri vilikamatwa kutokana na kukiuka sheria za forodha kwa kusafirisha bidhaa za magendo kutoka nchi jirani ya Kenya.  

Kwa mujibu wa meneja huyo, vyombo hivyo vya usafiri vilikamatwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 na kusisitiza taratibu za kisheria zinafanywa na mamlaka hiyo ikiwamo kutangaza kwenye vyombo vya habari kabla ya kuuzwa kwa njia ya mnada na fedha zitakazopatikana zitafidia kodi iliyokwepwa na wahusika.

Amesema TRA imeongeza jitihada katika kukabiliana na wimbi la uingizwaji wa bidhaa za magendo nchini kwa wafanyabiashara kuzingatia sheria na kwamba wimbi hilo limeanza kupungua kwa kiwango kikubwa licha ya kuwepo baadhi ya wafanyabiashara wanaoendelea na biashara hiyo.

Hivi karibuni TRA ilizindua kampeni ya operesheni ya nyumba kwa nyumba, duka kwa duka  kusaka watu wanaojihusisha na biashara za magendo hasa katika miji ya Tarakea na Holili ambako inakadiriwa uwepo za zaidi ya njia 300 za panya zinazotumika kupitisha bidhaa za magendo kutoka nchini Kenya.

“Kila mwaka TRA imekuwa ikiongeza jitihada kubwa kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinafuata sheria, hali ambayo imesababisha bidhaa za magendo kupungua kwa kiasi kikubwa huku changamoto kubwa ikiwa ni baadhi ya wafanyabiashara kuendelea na biashara hiyo,” amesema Iwato.

Meneja huyo amesema TRA itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara mbalimbali ili kutambua umuhimu wa kulipa kodi kwa manufaa ya taifa.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi, amesema mamlaka hiyo imeendelea kufanya operesheni ya mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba na duka kwa duka pamoja na kutoa elimu kwa walipa kodi pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili kwenye ulipaji wa  kodi.

Katika hatua nyingine, meneja huyo amedai kuwepo kwa zaidi ya leseni 10,000 za madereva wa vyombo vya moto ambazo zimerundikana katika ofisi hizo za TRA huku wahusika wakishindwa kuzichukua na baadhi yake zikiteketezwa kwa moto baada ya kwisha muda wake wa matumizi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mghwira ametoa wito kwa TRA kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ulipaji wa kodi pamoja na kufanya biashara halali ili kufikia Tanzania ya viwanda.   

Mghwira amesema jukumu la TRA si kuwekeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi pekee, bali  pia wana jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kuongeza wigo katika biashara, ikiwamo kufungua viwanda na kufanya biashara halali na kuzingatia sheria za nchi.