Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Awamu ya Pili ya utekelezaji wa Mfumo wa Mashine za Kielektroniki (ETR), kwa wafanyabiashara zaidi ya 200,000 wenye mauzo ghafi ya Sh milioni 14 kwa mwaka.
Akizungumza katika uzinduzi huo Dar es Salaam hivi karibuni, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kitaifa wa Serikali ya Denmark, Charlotte Slente, ameishauri TRA kutoa misamaha ya kodi inayolenga kuwapunguzia wananchi umaskini na kuleta usawa katika jamii.
Amesema Serikali ya Denmark inahakikisha misamaha ya kodi inasaidia katika kuweka usawa kwa kila mtumiaji, na kupunguza umaskini kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitillya, amesema dhamira hiyo itatekelezwa kwa kuboresha kumbukumbu za wafanyabiashara, kukuza ulipaji kodi kwa hiari na kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali.
Amesema Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa mfumo huo ilianza Julai 2010, ikiwahusu wafanyabiashara waliosajiliwa, na kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Kitillya amesema Awamu ya Pili inaanza na kundi la wafanyabiashara 200,000 wenye mauzo ya thamani ya Sh milioni 14, na kwamba mwaka wa kwanza makusanyo yaliyotokana na VAT yalikua kwa asilimia tisa na mwaka uliofuata yalikua kwa asilimia 23.
Kwa mujibu wa Kitillya, mashine hizo zimetengenezwa ili kumnufaisha mtumiaji katika uendeshaji wa biashara, ikiwa ni pamoja na uhakiki wa usalama wa taarifa za biashara yake, ambazo hutunzwa katika sehemu maalum bila kuharibiwa na mwingiliano wowote wa sumaku.
Faida nyingine ni kupata taarifa za mauzo kila siku kwa urahisi, kulingana na taarifa za bidhaa ambazo hazijauzwa, kumpa mtumiaji njia ya kisasa ya kutunza kumbukumbu za biashara.
Amesema ili kurahisisha upatikanaji wa mashine hizo, TRA imesaini mikataba na kampuni 11 zitakazosambaza, kufundisha watumiaji na kutoa huduma ya matengenezo.
Amezitaja kampuni hizo kuwa ni Advatech Offices Solutions Ltd, Business Machines Tanzania Ltd, Bolsto Solutions Ltd, Checknocrats Ltd, Compulynks Ltd, Maxcom Afrika Ltd, Pergamon Tanzania Ltd, Powercomputers and Telecommunications Ltd, SoftNet Technologies Ltd, Total Fiscal Solutions Ltd, na Web TECNOLOGIES Ltd.
Sambamba na wasambazaji wa mashine, kampuni nne zinasambaza karatasi zenye ubora, risiti zisizofutika ambazo zinatumiwa na mashine hizo. TRA imekuwa ikitoa mafunzo kwa makundi mbalimbali kama njia ya kuyatayarisha kwa ajili ya EFD.
Kitillya ameongeza kuwa Serikali imetaka gharama za ununuzi wa mashine hizi zitafsiriwe kama gharama za biashara, na mtumiaji ataruhusiwa kupunguza gharama hiyo mara moja kwa mwaka wa kwanza wa kutumia mashine, ambapo bei ya mashine moja ni Sh 800,000.
Amewataka Watanzania kujenga tabia ya kuomba risiti au ankara kila wanaponunua bidhaa au huduma, na kwamba majukumu hayo yataiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii kwa urahisi na hatimaye kuboresha maisha ya Watanzania walio wengi.
Naye Kamishna wa Kodi za Ndani, Patrick Kasera, amezitaja changamoto walizokutana nazo katika Awamu ya Kwanza kuwa ni pamoja na wafanyabiashara kutokuwa na elimu ya kutosha kutoka kwa wasambazaji kuhusu matumizi ya mashine hizo.
Pia kulikuwapo na tatizo la kufutika haraka kwa karatasi zinazotumiwa na mashine hizo na mashine nyingine zikuwa ghali.
Ameongeza kuwa kuingia Awamu ya Pili kumezingatia hatua mbalimbali za kuondoa changamoto hizo.
“Tumeongeza idadi ya watengenezaji wa mashine kutoka wanne hadi wanane na wasambazaji kutoka sita hadi 11, ili kuhakikisha huduma ya matengenezo inapatikana kwa urahisi nchi nzima.
“Mashine zinazokidhi viwango tunavyohitaji zimeshawasili hapa nchini tayari kuuzwa kwa wafanyabiashara, kwa hiyo baada ya ufunguzi huu wafanyabiashara wanaweza kwenda kuzinunua kwa wasambazaji,” amesema Kasera.
Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Maxcom (MaxMalipo), Ahmed Lussasi, amesema wako tayari kukabiliana na changamoto zozote, kwani wamesambaa nchi nzima.
“Tumejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na TRA katika kutoa huduma hizi kwa wafanyabiashara wote hapa nchini, na kwa viwango vinavyokubalika,” amesema Lussasi.