Huenda Watanzania wataanza kunufaika ipasavyo na rasilimali za nchi, ikiwa Bunge litaridhia hoja ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) inayotaka ianzishwe sera ya upendeleo maalum kwa wazawa katika ugawaji zabuni na maeneo ya uwekezaji.

Sera hiyo inalenga kuwaongezea wazawa fursa ya kumiliki uchumi utakaowawezesha kuaga umaskini, tofauti na hali ilivyo sasa ambapo wengi wao hawamudu ushindani unaowashirikisha wageni katika kugombea zabuni na uwekezaji.

 

Iwapo TPSF itafanikiwa kutetea hoja hiyo hadi iridhiwe na Bunge, basi ule msemo kwamba kuzaliwa maskini si kosa bali kuishi na kufa maskini ndiyo kosa, utadhihirika wazi miongoni mwa Watanzania.

 

TPSF inakazana kupendekeza sera hiyo sambamba na kuandaa maoni yatakayotetea suala hilo kwenye mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao chao Dar es Salaam hivi karibuni, viongozi wa Bodi ya TPSF walisisitiza kuwa huu ni wakati mwafaka wa kubadilisha utaratibu wa kumshindanisha mzawa na wageni, ambao kimsingi hawezi kuwashinda katika kupata fursa za kiuchumi.

 

“Tunaangalia namna gani Mtanzania atamiliki uwekezaji kwenye rasilimali kubwa, lakini pia asishindanishwe na watu [wageni] asioweza kushindana nao,” amesisitiza Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Salum Shamte.

 

Shamte anataja moja ya rasilimali kubwa ambazo Mtanzania anastahili kuzitumia kujikomboa kiuchumi kuwa ni ardhi kwa ama kuimiliki kiuwekezaji, au kuingia ubia na wageni.

 

“Tunataka Watanzania wafaidike moja kwa moja na rasilimali za nchi, hili linafanyika katika nchi nyingi, na linawezekana hata hapa kwetu [Tanzania]. Tunataka kila shughuli ya kiuchumi hapa nchini Mtanzania awemo,” anaongeza.

 

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya TPSF, Dk. Reginald Mengi, ametetea hoja hiyo akisema ndiyo njia pekee itakayowapatia wazawa fursa ya kunufaika ipasavyo na neema ya rasilimali lukuki nchini.

 

Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa 14 wa TPSF uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni. Ataitumikia taasisi hiyo kwa wadhifa huo kwa kipindi cha miaka miwili.

 

Anasema Serikali inastahili pongezi kwa kuona umuhimu wa sekta binafsi kuwa na sauti moja, lakini akasisitiza kuwa sauti hiyo haitakuwa na maana kama haitapigania fursa za kuwawezesha wazawa kunufaika ipasavyo na rasilimali za nchi.

 

“Sauti moja ya sekta binafsi itachangia kuwawezesha wazawa kumiliki na kudhibiti rasilimali za Taifa. Tunataka sheria ya ununuzi wa umma iangaliwe upya, ikibidi Watanzania ndiyo wapewe tender hizi kwani ndiyo njia kuu itakayowawezesha kiuchumi,” anasema Dk. Mengi.

 

Kwa mujibu wa Dk. Mengi, ukosefu wa sauti moja ya sekta binafsi nchini ulisababisha sekta hiyo kuyumba miaka mitatu iliyopita, lakini sasa imepata matumaini ya kuanza kuimarika kwa kasi mpya.

 

Anafafanua kuwa juhudi hizo zinalenga kuwajengea wazawa mazingira rafiki ya kunufaika pia na asilimia karibu 80 ya pato la Taifa inayoelekezwa kwenye sekta ya ununuzi wa umma (public procurement).

 

“Mwaka huu [2013] karibu [shilingi] trilioni 14 zimeelekezwa kwenye ununuzi wa umma. Hizi fedha kama wangepewa Watanzania wangepata faida asilimia 10 ambayo ni sawa na [shilingi] trilioni 1.3.

 

“Tunataka ununuzi wa umma uwe chombo muhimu cha kuwawezesha Watanzania kiuchumi. Siyo kwamba Watanzania  hawawezi, wanaweza sana, suala ni kuwawezesha,” anasisitiza Dk. Mengi.

 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TPSF anafafanua kuwa kimsingi msimamo wa taasisi hiyo haulengi kuzuia wageni kuwekeza hapa nchini, bali kuhakikisha wazawa wananufaika pia na uwekezaji wa kigeni kwa kiwango kinachoridhisha.

 

Huku akionekana kuzungumza kwa kujiamini zaidi, Dk. Mengi amesema taasisi hiyo inawategemea wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanikisha uanzishwaji wa sera ya kuwapa wazawa upendeleo maalum katika uwekezaji wa kiuchumi.

 

Akijibu swali lililoulizwa na JAMHURI kutaka kujua kama msimamo huo wa TPSF hautajenga taswira ya kuwabagua wawekezaji katika mahitaji ya uwekezaji na zabuni zikiwamo za ununuzi wa umma, Dk. Mengi amesema jambo hilo ni la kawaida duniani.

 

“Hakuna nchi yoyote duniani ambayo haipendelei wananchi wake. Tatizo lililopo ni kwamba Watanzania wanaona aibu kusema ‘tunapendelea Watanzania’. Tunapaswa kuwa na sera ya kuwapendelea wazawa badala ya kuwapendelea wageni katika uwekezaji kwenye rasilimali za Taifa,” anasisitiza.

 

Akisisitiza zaidi, Dk. Mengi anasema, “Upendeleo utakaowawezesha Watanzania kunufaika kikamilifu na rasilimali za nchi yetu ni haki yetu ya kuzaliwa Tanzania, hakuna ubaguzi hapa.”

 

Kwa upande mwingine, Dk. Mengi ameeleza kushangazwa kwake na Watanzania wanaoendelea kukumbatia mtazamo hasi, ambao bado wanaamini kimakosa kwamba hawawezi kufanya lolote na kufanikiwa kiuchumi bila kusaidiwa na Wazungu.

 

“Waandishi wa habari tusaidieni kuwatia nguvu Watanzania. Ifike mahali Watanzania tujiamini kuwa tunaweza. Tusiache rasilimali zetu zitumike sisi tumelala,” anasema.

 

Akizidi kutetea hoja hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Salim Shamte, anasema hakuna sababu ya Watanzania kulionea aibu suala la kujipendelea katika ugawaji wa zabuni na maeneo mengine ya kuwekeza kiuchumi kwa kuwa jambo hilo linatazamwa kama ujasiri duniani.

 

“Utaratibu huu ni uamuzi mzuri wa kutaka kuwawezesha Watanzania wakue kiuchumi,” anasisitiza Shamte.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, amekosoa utaratibu wa sasa wa Serikali kuwapendelea wageni katika uwekezaji kwenye rasilimali muhimu za nchi, akisema dhana hiyo hailengi kuwezesha maisha bora kwa kila Mtanzania.

 

“Kwa mfano, Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi asilia maeneo ya Kusini [mkoani Mtwara] lakini waliopewa leseni za kuvuna utajiri huo ni wageni wanaomiliki kampuni kubwa,” anasema.

 

Simbeye anadokeza kuwa TPSF haijakaa kimya katika kushughulikia suala hilo kwani tayari imeshaandaa rasimu ya mwisho ya gesi asilia na kuipeleka Wizara ya Nishati na Madini. Rasimu hiyo inataka wazawa wapewe kipaumbele katika kunufaika na nishati hiyo.

 

“Mbali ya kunufaika na gesi asilia, tunataka iwepo pia sera inayoelezea jinsi Mtanzania atakavyokuwa anashirikishwa katika ugawaji wa vitalu vya uwekezaji wa kitalii nchini,” anasema Simbaye.

 

TPSF ilianzishwa Novemba 1998 kutokana na msukumo wa wadau mbalimbali wa sekta binafsi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

 

Bodi mpya ya TPSF inaundwa na Dk. Reginald Mengi, Salum Shamte, Godfrey Simbeye, Felix Mosha, Dk. Gideon Kaunda, Dk. Charles Kimei, Deo Mwanyika, Enock Ndondole, Mbarouk Omar Mohamed, Anna Matinde, Gaudence Temu na Mhandisi Peter Chisawilo.

 

Ahadi kubwa ya taasisi hiyo ni kwamba itaendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga uchumi imara kwa Watanzania.