Katika juhudi za kuisaidia Serikali kukabili mabadiliko ya tabianchi, Benki ya Posta Tanzania (TPB) imetenga Sh milioni sita kugharamia upandaji miti mkoani Mwanza.
Meneja wa TPB Tawi la Mwanza, Shaban Telatela, amethibitisha hayo katika hafla ya upandaji miti 1,200 kutunza mazingira ya Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, mkoani hapa.
Benki hiyo inatekeleza mpango huo chini ya utaratibu iliojiwekea wa kutumia sehemu ya faida inayopata katika utoaji huduma za kibenki, kuchangia maendeleo ya jamii yanayojumuisha sekta za mazingira, afya na elimu.
“Benki yetu {TPB} inaamini utunzaji mazingira ukiwamo upandaji miti, utasaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Hii miti tuliyoipanda hapa hospitalini ni mwendelezo wa mikakati yetu, na hatutarudi nyuma,” amesisitiza Telatela.
Katika hatua nyingine, meneja huyo ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza kujiunga na benki hiyo, kuiongezea uwezo wa kuchangia zaidi maendeleo ya wananchi na Taifa kwa jumla.
Inaelezwa kuwa TPB inaendelea kuboresha zaidi huduma za kibenki, zikiwamo za kupitia simu za mkononi kwa wateja wake ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikillo, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amezihimiza halmashauri za jiji, manispaa na wilaya mkoani kuhakikisha zinatekeleza sera ya nchi ya kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
Huku akipongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa TPB kuchangia maendeleo ya wananchi na Taifa, Ndikillo amezitaka idara za Mazingira na Misitu kuongeza kasi ya kudhibiti vitendo vya uvamizi wa misitu na ukataji miti ovyo.
“Mikakati hii itasaidia kuuepusha mkoa wetu {Mwanza} na Taifa letu kukumbwa na jangwa,” amesema kiongozi huyo wa mkoa.