Na Mwandishi Wetu JamhuriMedia, Dar es Salaam
SEKTA za Uchukuzi na Usafirishaji zimetakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana ili ziweze kuwa na tija katika kuongeza kasi ya ukuaji uchumi hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Masoko Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bi Fatma Adadi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa mamlaka hiyo Dkt. George Fasha kwenye Mkutano huo wa pili wa Uchukuzi na Usafirishaji – unaojulikana kama East Africa Cargo Connect Summit uliofanyika mwishoni jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo mkubwa wa siku moja uliwakutanisha wadau wa sekta ya uchukuzi wa sekta ya maji, anga, reli na barabara kujadaliana changamoto zinazowakabili na utatuzi wake ili kuangalia kwa namna gani zinaweza kuchochea ukuaji wa soko la ajira na uchumi.
Bi. Fatma aliwapongeza wadau wa uchukuzi na usafirishaji kwa kuandaa mkutano huo na kuwasisitiza umuhimu wa kukutana mara kwa mara ili kujadili mafanikio na changamoto zinazoikumba sekta hizo.
“Nitumie nafasi hii kuwasisitiza umuhimu wa kukutana mara kwa mara na kuzungumzia sekta yenu ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwenye kukuza uchumi kwa njia ya usafirishaji na uchukuzi,”
“Sisi (TPA ) kama wadau muhimu tutaendelea kushirikiana na nyie kila wakati katika kuhakikisha tunasaidia ukuaji wa uchumi hapa nchini,” alisema.
Ofisa Masoko huyo alisema kupitia vikao hivyo vya majadiliano wadau watakuwa wanatoka na maazimio chanya yatakayoleta mchango mkubwa wenye kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za uchukuzi zikiwemo za kibandari.

Aidha Fatma amewataka wadau wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji kuiboresha sekta hiyo na kuhakikisha utoaji huduma unaendelea kuwa bora zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya EB Maritime, Emmanuel Mallya ambaye alipewa Tuzo ya Lifetime Achievement, alisema katika mnyororo wa sekta hiyo kuna maeneo manne muhimu yanapaswa kutambulika, ambayo ni wamiliki wa meli, mamlaka ya bandari, wamiliki wa mizigo na mamlaka za kikodi.
Mallya alisema kupitia maeneo hayo manne sekta ya bandari hasa Tanzania imekuwa nzuri, hivyo kuwezesha sekta zingine kama reli, barabara na bandari kavu kufanya kazi vizuri na kwa faida.
Alisema mkutano huo una nafasi kubwa ya kuwafanya wajadiliane na kutoka na matokeo chanya ambayo yataleta mabadiliko kwa haraka.
“Sisi tumekutana hapa kwa siku moja tunapaswa kutoka na suluhisho ambalo litaleta mabadiliko kwenye sekta hii muhimu kwenye uchumi wa nchi,” alisema.
Kupitia mkutano huo ambao umedhamiwa na TPA na kushirikisha wadau wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji kutoka nchi za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) na Afrika Magharibi, tuzo mbalimbali za umahiri zilitolewa.
Katika tuzo hizo,Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alipewa tuz Kiongozi Mahiri mwenye maono katika Sekta ya Uchukuzi kwa Njia ya Maji “The Tanzania Maritime Visionary Leadership Award”