Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA imewakikishia Wadau wa Sekta ya Madini Nchini kuendelea kuhudumiwa kwa Weledi na ufanisi wakati wote wa kusafirisha nje ya Nchi au kuingiza Nchini bidhaa na malighafi za Sekta ya Madini.
TPA inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Tano ya Sekta ya Madini yanayofanyika Mkoani Geita yakishirikisha Wadau wa Sekta ya Madini wa ndani na nje ya Nchi na kuhudhuriwa na maelfu ya Wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TPA Bw Nicodemus Mushi amesema, TPA imetumia vyema maonesho haya kukutana na wadau muhimu wa Sekta ya Madini ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa kiwango cha Shehena zinazopita katika Bandari za Tanzania na hasa Bandari kuu ya Dar es Salaam
Uhusiano wa TPA na shughuli za Madini ni mkubwa sana, tunategemeana kwa kiasi kikubwa. Bidhaa za Madini, Mitambo na Malighafi za uchimbaji ni Shehena muhimu zinazopita katika Bandari zetu.
Wakati Sekta ya Madini ikitegemea Bandari katika usafirishaji, TPA inategemea shehena hii katika kuingiza mapato yake kupitia biashara ya Bandari kwa ujumla.Tanzania inahudumia Nchi nane majirani kupitia Bandari zake na hasa Bandari ya Dar es Salaam huku Nchi zenye utajiri wa Madini kama Congo na DRC na Zambia ni Wateja Wakuu wa TPA.
Katika mipango yetu ya muda mfupi na mrefu, tutaendelea kushirikiana na Wadau wa Sekta hii ya madini ili kuhakikisha kuwa, wanapata huduma bora, usalama wa uhakika na gharama nafuu kulingana na mahitaji yao wakati wote.
Pamoja na maonesho haya kutawaliwa na shughuli za Madini, Wananchi waliotembembea Banda la TPA wameonesha shauku kubwa ya kufahamu shughuli za Mamlaka hii hasa huduma za kuagiza Magari na Mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Bandari kuhusu uendeshaji wa shughuli za Meli na Bandari, uingizaji na utoaji wa mizigo Bandarini, taratibu za usafirishaji ndani ya maji, matengenezo ya vyombo pamoja na mafunzo ya zimamoto na uokoaji.
Chuo cha Bandari ni miongoni mwa Vyuo bora Nchini katika kutoa elimu inayowaandaa Vijana kufanya kazi katika Sekta ya Huduma za Kibandari kama vile uendeshaji wa vyombo vinavyotumika kupakia na kupakua mizigo Bandarini.
Kwa upande wao Wadau wa sekta ya Madini wameipongeza Serikali kwa kuiwezesha TPA kukamilisha miradi kadhaa ya Upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na kukamilika kwa ujenzi wa Bandari mpya ya Karema.
Wakala wa Madini anayefanya shughuli zake kati ya Tanzania na Zambia Bw Felix Wambali anasema, kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Karema ni mafanikio makubwa kwa Taifa la Tanzania, kwani bandari hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika Maendeleo ya sekta ya Bandari na Uchumi wa Taifa.Bandari ya Karema ni habari njema sana kwetu Wafanyabiashara, umbali kati ya Karema na Mji wa Kibiashara wa Kalemii ni mfupi sana na kwa kutumia Bandari hiyo, tutaokoa muda na kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni gharama za usafirishaji.
Wambali anazishauri Serikali za Tanzania na Congo kuunganisha nguvu zao ili kujenga miundombinu ya kibandari upande wa Congo kwani kwa upande wa Tanzania, kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa miundombinu ya Kibandari hali inayohitaji uwekezaji kama huo kufanyika pia upande wa pili ili kuwezesha biashara ya usafirishaji kufanyika.