Na Mwandishi Wetu, JamhuriMesia, Dar es Salaam

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeibuka mshindi wa tatu katika kundi la taasisi za Umma zinazozingatia na kufuata miongozo na kanuni za Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-Ga) katika uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA katika shughuli zake.

TPA imepata jumla ya asilimia 91.11 katika tathmini ya uzingatiaji wa kanuni na miongozo inayotolewa na e-GA katika uendeshaji wa Serikali Mtandao.

Ushindi wa TPA unatokana na uboreshaji huduma katika bandari inazozisimamia hapa nchini ikiwemo bandari ya Dar es Salaam ambapo utoaji huduma ukiwemo upakiaji na ushushaji mizigo imeongezeka na kuvutia wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni, Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi ikiwemo ya Jamhuri ya Congo ( DRC) walitembelea bandari hiyo na kuvutiwa na utendaji kazi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa kutumia teknolojia ya kisasa katika utoahi huduma na kuwafikia wateja (Customer Care).

TPA chini ya Mkurugenzi Plasduce Mbossa imefanya maboresho katika bandari mbalimbali ikiwemo ya Mbamba Bay , Tanga, Mtwara na nyinginezo katika kukuza ukuaji wa biashara na uchumi.

Mbali na utoaji wa tuzo hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Bw George Boniface Simbachawene( Mb) pia alifunga Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao, tarehe 13 Februari, 2025 jijini Arusha na kuwaelekeza viongozi na watumishi wa umma kuzingatia na kutekeleza maazimio 6 ya kikao hicho ipasavyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene( kushoto) akikabidhi tuzo ya Mshindi wa tatu katika kundi la Taasisi za Umma zinazozingatia na kufuata Miongozo na Kanuni za Mamlaka ya Serikali Mtandao katika uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA kwa Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Abdullatif Minhaji, wakati wa kugungwa kwa Kongamano la 5 la Serikali Mtandao, tarehe 13 Februari,2025, Jijini Arusha.

Bw Simbachawene amehimiza umuhimu wa kutekeleza maazimio hayo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuboresha huduma za Serikali kwa wananchi wake kwa mifumo ya kidigitali.

Kongamano hilo lililokuwa na Kauli Mbiu “ Huduma za Serikali Mtandao na ubunifu wa Utoaji Huduma za Mifumo ya TEHAMA kwa wananchi kwa ufanisi” limejadili jitihada za e-GA katika kujenga Serikali mtandao.

Masuala mengine yaliyojiri katika kikao hicho ni kubainisha fursa na changamoto za utekelezaji Serikali Mtandao pamoja na mbinu bora za kufanikisha na kuendesha Serikali Mtandao.

Kongamano la 5 la Mwaka la Serikali Mtandao limehudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Mamlaka za umma, Sekta Binafsi na Wataalamu kutoka nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Huduma za TEHAMA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Abdullatif Minhaji ( Kushoto) akitoa maelezo mbalimbali kuhusu uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya TEHAMA katika kazi za utoaji huduma zenye ufanisi Bandarini, kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene( Mwenye suti Nyeusi katikati) kabla ya kufungwa kwa Kongamano la 5 la Serikali Mtandao, tarehe 13 Februari,2025, Jijini Arusha.