Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Chuo cha Arab Academy for Science Technology and Maritime Transport (AASTMT) cha nchini Misri zimesaini randama ya makubaliano ya kushirikiana katika kutoa mafunzo ya shughuli za kibandari kwa Wafanyakazi.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kusaini randama ya makubaliano hayo yakishuhudiwa kundi la kwanza la wafanyakazi 23 waliopata fursa ya kwenda kusoma fani za uhandisi wa baharini na uendeshaji meli katika Chuo hicho,Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw Plasduce Mbossa amesema makubaliano hayo ni sehemu ya mpango wa mamlaka wa kuwaendeleza wafanyakazi,kuongeza ufanisi pamoja na kuifanya TPA kuwa sehemu sahihi.
“Makubaliano haya ni kielelezo cha dhamira ya TPA kutaka kuwaendeleza wafanyakazi wake wawe na ujuzi na maarifa stahiki katika uendeshaji na ufanyaji wa kazi za bandari,” alisema Bw Mbossa.
Alisema TPA imejipanga kuendeleza uwezo wa wafanyakazi wake katika kutoa huduma maeneo yote muhimu ya ndani ya maji na ardhini ni jambo muhimu sana katika kutanua shughuli zetu za utoaji huduma kwa wateja wanaotumia bandari zetu,”
“Makubaliano haya yatawezesha wafanyakazi wetu kupata mafunzo katika chuo hicho nchini Misri chenye uzoefu wa masuala yanayohusu bandari ili kuwajengea uwezo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari zetu hapa nchini,” amesema Bw Mbossa.
Amesema TPA imeamua kuingia makubaliano na chuo hiki kwa sababu ya uzoefu wake katika kutoa mafunzo yenye ubora wa ngazi za kimataifa.
“Tuliangalia vyuo vingi, lakini tuliamua kuingia makubaliano na chuo hiki cha Misri baada ya kuridhishwa na weledi sambamba na uzoefu wake,”alisema bosi huyo wa TPA na kuongeza kuwa
“Tumekuwa na mahusiano na chuo hiki kwa muda mrefu ambapo katika miaka ya nyuma tulipeleka manahodha wetu wa meli na wafanyakazi wengine wa idara mbalimbali kupata mafunzo ya kuongeza ufanisi na mafunzo mengine ni ya ulazima katika kuhuisha vyeti vyao,” amesema Mbossa.
Amesema vijana watakaokwenda kupata masomo ya muda mrefu katika chuo hicho kwa sasa ni wale wenye elimu ya kidato cha sita ambao wataongezewa ujuzi na kupata vyeti ili kutoa huduma bora katika bandari mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Chuo hicho,Prof Ismail Abdelghaffar amesema kwa kusaini makubaliano haya,taasisi hizi mbili zinaanza safari mpya ya pamoja kuelekea kutimizi ndoto na matarajio ya pamoja kitaaluma.
“Nimefurahi sana na nina heshima kubwa kukutana na viongozi wa kipekee wa sekta ya baharini hapa Tanzania,”
“Dira yao, mikakati yao, kazi yao, kujitolea kwao, na imani yao katika kuwekeza katika rasilimali watu ni muhimu sana kwa mustakabali wa sekta hii muhimu ya baharini,” amesema Prof Abdelghaffar.
Ameongeza kuwa chuo chao kitafanya kazi kwa pamoja na TPA katika kukuza rasilimali watu wa baadaye kwa sekta hii.
“Ufanisi na uweledi wa bandari utazidi kuongezeka kwa kuwa na watoa huduma wenye ujuzi na hadhi ya kimataifa,” alisema na kuwa
ni muhimu sana katika mahitaji ya soko la ushindani kwa sasa.
TPA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuongeza ufanisi wa utendaji katika bandari zake ambapo Umoja wa Wafanyabishara nchini Tanzania (UWT) hivi karibuni walitembelea katika bandari ya Dar es Salaam kujionea uwekezaji mkubwa uliofanyika na kuridhishwa na matokeo yake makubwa ya kasi ya kushusha na kupakia mizigo kwa mitambo ya kisasa.