Na Mwandishi Maalum
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefungua ofisi katika Jiji la Kigali nchini Rwanda itakayotoa huduma zote za Bandari. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa ndiye amefungua ofisi hii hivi karibuni.
Waziri Mbarawa amesema lengo la Serikali ya Tanzania kufungua ofisi hiyo ni jitihada za TPA kusogeza huduma za bandari karibu na wateja wake nchini Rwanda kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za kibandari.
Katika hafla ya ufunguzi wa ofisi hiyo ambayo ilihudhuriwa na Waziri wa Uchukuzi wa nchi ya Rwanda, Mheshimiwa Jean de Dieu na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mheshimiwa Ali Iddi Siwa, Mbarawa ametanabaisha kwamba kufunguliwa kwa ofisi ya TPA jijini Kigali ni ishara tosha kuwa serikali ya Tanzania imedhamiria na imejidhatiti kuhakikisha biashara kati ya Tanzania na Rwanda inafanyika bila vikwazo kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Mbarawa ameishukuru Serikali ya Rwanda na Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa kuiunga mkono na kuiwezesha TPA hadi kukamilisha shughuli za ufunguzi wa ofisi. Pamoja na kuwa na uhusiano wa karibu kati ya Tanzania na Rwanda kuzidi kuimarika, mizigo ya Rwanda itahudumiwa kwa haraka na kwa wepesi zaidi. Ofisi hii ya TPA jijini Kigali itajumuisha huduma zote zikiwemo za utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na taarifa za wadau wa bandari.
Pia amesema Tanzania imeboresha mazingira ya kufanya biashara nchini Tanzania kwa wafanyabiashara wa Rwanda kuimarisha miundombinu na huduma zinazotolewa katika sekta mbalimbali. Kituo cha huduma cha ushuru na forodha wa pamoja cha Rusumo ni muhimu sana kwa Tanzania katika kuboresha na kuimarisha ufanyaji biashara kwani kazi kubwa ya kituo hicho ambacho kinafanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki kuharakisha upitishaji wa mizigo kutoka Tanzania kwenda Rwanda au kutoka Rwanda kwenda Tanzania.
Mbarawa aliwafahamisha Wanyarwanda kwamba, kwa sasa serikali ya Tanzania ipo katika mpango wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa kujenga Reli ya Kisasa (Standard Gauge Railways – SGR) kati ya Tanzania na Rwanda ili wafanyabiashara waweze kusafirisha mizigo yao kwa urahisi na kwa haraka hata abiria nao wataweza kusafiri kwa haraka.
Naye Waziri wa Uchukuzi wa Rwanda, Mheshimiwa Jean De Dieu akiongea katika hafla hiyo alisema kufunguliwa kwa ofisi ya TPA kutarahisisha usafirishaji wa mizigo ya Rwanda kwa haraka zaidi na kuwawezesha wafanyabiashara kupata mizigo yao kwa haraka. Hatua hiyo itaiwezesha bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa urahisi na ufanisi mkubwa. Urahisi wa kusafirisha mizigo kwa haraka utapunguza gharama za kufanya biashara kwa watu wa Tanzania na Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Dieu alisema pamoja na kufunguliwa kwa ofisi ya TPA nchini Rwanda, Kituo cha huduma cha pamoja cha ushuru na forodha cha Rusumo kimesaidia sana kuongeza kasi ya huduma wa mizigo kuwa ya ufanisi mkubwa. Kituo hicho kimewezesha hali ya kibiashara kuongezeka sana kati ya Tanzania na Rwanda baada ya kuondolewa kwa vituo vya barabarani visivyo vya kiforodha (check points) kuanzia Dar es Salaam hadi Rusumo.
Kwa upande Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mheshimiwa Ali Iddi Siwa, aliishukuru Serikali ya Rwanda, Jumuiya wa Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kwa kuiunga mkono Bandari ya Dar es Salaam kupitisha shehena ya mizigo ya nchi yao hali ambayo imefanya mizigo ya Rwanda kupitia Dar es Salaam kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Kuongezeka kwa mizigo ya Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam kumekuwa kichocheo kwa serikali ya Tanzania kufungua ofisi ya TPA nchini Rwanda kwa lengo la kuwasogezea huduma za kibandari wafanyabiashara wa Rwanda. Kuongezeka kwa kasi ya biashara kati ya Tanzania na Rwanda kumeongeza hamasa ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kimaendeleo kwa nchi mbili hizi.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa ofisi ya TPA nchini Rwanda, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema Bandari ya Dar es Salaam inahudumia asilimia 90 ya biashara yote ya bandari kwenye Bahari ya Hindi ukilinganisha na bandari nyingine za Tanzania zikiwamo za Tanga na Mtwara. Amesema TPA imeendelea kuboresha utoaji huduma katika Bandari ya Dar es Salaam kama vile TEHEMA na ulinzi ambapo TPA imeweka mfumo wa kisasa wa ulinzi wa Integrated Security System kwa lengo la kuhakikisha mizigo ya wateja inakuwa salama.
Kakoko ametanabaisha kuwa ofisi hiyo ya TPA itawasaidia wafanyabiashara wa Rwanda kutatua changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za mizigo yao kupitia bandari ya Dar es Salaam. Pia ofisi hiyo itawasaidia wafanyabiashara na wateja wa bandari nchini Rwanda kuepuka kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kufuatilia shehena za mizigo yao inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Pia Kakoko amesema Rwanda ni nchi inayoongeza kwa usafirishaji wa mizigo yake kupitia Bandari ya Dar es Salaam miongoni mwa nchi jirani zinazotumia Bandri ya Dar es Salaam. Mzigo wa Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kutoka tani 629,938 mwaka 2014 hadi tani 1,200,000 mwaka 2017 na kuifanya kuwa nchi wa tatu miongoni mwa nchi zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam.
Kakoko aliwafahamisha Wanyarwanda kwamba, TPA ipo katika utekelezaji wa mradi mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam ujulikanao Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) ambao unahusisha uongezaji wa kina cha gati kuanzia namba 1 – 11, kuongeza kina na upana wa mlango wa bandari (entrance channel) hadi kufikia mita 15, kujenga gati maalumu ya meli za magari (RO-RO), kujenga gati nne za kitengo cha makasha na kujenga gati ya kisasa ya kuhudumia shehena ya kichele na kuboresha ghala la nafaka. Mradi huo utakapokamilika utaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia meli kubwa (panamax vessels) na shehena ya mizigo kubwa zaidi.
Kwa upande wake Kapteni Dieudonne Dukundanne, Katibu Mtendaji wa Shoroba ya Kati (Central Corridor), ameziomba serikali zinazotumia Shoroba ya Kati kupitishia mizigo yao katika Bandri ya Dar es Salaam kupunguza gharama za mawasiliano na uchukuzi wa mizigo ili kuwasaidia watu kufanya biashara kwa haraka, ufanisi na faida kwa maslahi mapana ya kujiletea maendeleo makubwa.
Je, kuna jambo unataka kuiambia TPA? Ikiwa una kero, ushauri au maoni tuma ujumbe (sms) au piga simu bure kupitia namba 0800110072 na 0800110073, barua pepe; [email protected], barua kwa njia ya posta kwa anuani; Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, S. L. P 9184, Dar es Salaam. Bandari pia inawasikiliza wananchi wanaofika katika ofisi za Mamlaka kwa njia ya msaada au ushauri zaidi. Tushirikiane.