Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imekamilisha kazi ya kufunga mitambo miwili ya kisasa ya kufundishia kwa vitendo (Full Mission Crane Training Simulator) katika Chuo chake cha Bandari kilichopo Wilaya ya Temeke, katika Mtaa wa Mahunda.
Mitambo hiyo ambayo imeanza kutumika kutoa mafunzo kwa vitendo inatarajiwa kutatua changamoto waliyokuwa wakikumbana nayo wanafunzi ya kupata fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo mara baada ya kukamilisha mafunzo ya nadharia darasani.
Akizungumza hivi karibuni mara baada ya kuzindua mitambo hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye amesema usimikwaji wa mitambo hiyo ni hatua kubwa iliyofikiwa na TPA na serikali kwa ujumla katika kuhakikisha Chuo cha Bandari kinafanya mabadiliko na maboresho katika utoaji wa taaluma ya shughuli za bandari kwa weledi mkubwa.
Waziri Nditiye amesema: “Serikali inafuatilia kwa karibu utendaji na maendeleo ya taasisi zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na Chuo cha Bandari. Tunazo taarifa kuhusiana na juhudi zinazoendelea za kuboresha chuo hiki, hii ni pamoja na kufahamu kwamba tayari mmepata ithibati kamili baada ya kuikosa kwa muda mrefu.”
Naibu Waziri ameongeza kwamba ni vema chuo kikakamilisha mapema kazi ya kupitia upya mitaala yake kwani iliyopo inahitaji kuhuishwa sambamba na kuandaa mitaala mipya ili kukidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira hususan itakayokidhi mahitaji ya serikali ya kuinua uchumi wa viwanda.
“Nakuhimiza wewe Mkuu wa Chuo kuendelea kutekeleza miongozo na maelekezo ya Bodi ya Wakurugenzi ya TPA ipasavyo na Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kufuatilia utendaji na maboresho ya chuo ili lengo la kufikia ufanisi wa utendaji wa wanafunzi wanaohitimu katika chuo hiki litimie,” ameongeza Nditiye.
Tayari Chuo cha Bandari kimekamilisha uandaaji wa Mpango Kamambe (Master Plan) wake wa miaka kumi na mbili sambamba na Mpango Mkakati (Strategic Plan) wa miaka mitatu, lengo likiwa ni kukifanya chuo kuwa cha kisasa, chenye kutoa mafunzo bora kwa sekta nzima ya usafirishaji kwa njia ya maji hapa nchini.
Akizungumzia suala la muda mrefu la urejeshwaji wa miundombinu na majengo ya Chuo cha Bandari kutoka Chuo cha Utalii, Naibu Waziri amesema kwamba wizara inayo taarifa kuwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TPA imo katika mazungumzo na Chuo cha Utalii pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto iliyopo na kuagiza kazi hiyo ikamilike kwa wakati uliopangwa.
Awali akizungumzia suala hilo mbele ya Naibu Waziri, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, aliiomba serikali na wizara kusaidia kukamilisha urejeshwaji wa miundombinu na majengo hayo ili kukiwezesha chuo kufundisha vijana wengi zaidi taaluma ya mambo ya Bandari.
“Bodi ya chuo ilipokea taarifa ya utendaji na kubaini kuwa kuna mapungufu makubwa katika eneo la miundombinu hususan madarasa, ofisi za wakufunzi na maafisa utawala wa chuo, hali hii imetokana na uamuzi wa serikali uliofanywa mwaka 2001 wa kugawa sehemu kubwa ya majengo ya Chuo cha Bandari kwenda Chuo cha Hoteli na Utalii ambacho kwa sasa tayari kimeshajenga jengo lake,” amesema Mhandisi Kakoko.
Ameongeza kuwa ugawaji huo wa majengo ya Chuo cha Bandari unaweza kukwamisha utekelezaji wa Mpango Kamambe uliondaliwa endapo majengo hayo hayatarejeshwa kutoka Chuo cha Utalii. “Tayari kamati iliyoundwa kwa kuhusisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Maliasili na Utalii ilipendekeza Chuo cha Utalii kihame na kurejesha majengo kwa Chuo cha Bandari, tunaomba sasa mapendekezo haya yatekelezwe katika kipindi kifupi kwa ajili ya kuongeza tija na ufanisi kwa chuo chetu,” amesema Mhandisi Kakoko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dk. Joseph Kakeneno, amesema katika mwaka wa masomo ulioanza Oktoba 2019, chuo kimedahili jumla ya wanachuo wapya 317 katika fani nne tofauti ambazo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za uhandisi na matengenezo, usimamizi wa utekelezaji bandarini, uwakala wa ushuru na forodha na usafirishaji na uchukuzi.
Mpaka sasa Chuo cha Bandari kina jumla ya wanafunzi 532 na inatarajiwa kwamba udahili wa mwezi Machi 2020 utaongeza idadi ya wanafunzi kufikia zaidi ya 800 huku kukiwa na mipango ya baadaye ya kutoa Stashahada za juu na Shahada katika taaluma za usafirishaji kupitia njia ya maji.
Hivi karibuni Februari 14, 2020 jumla ya wahitimu 403 wamehitimu katika Mahafali ya 18 ya chuo hicho ambapo kati yao wahitimu 143 wamehitimu Stashahada huku wahitimu 260 wamehitimu Astashahada katika fani mbalimbali za shughuli za Bandari.
Chuo cha Bandari kilianzishwa mwaka 1980 kwa lengo la kutoa mafunzo ya ndani kwa wafanyakazi wa TPA. Hatua ya kuanzishwa kwa chuo hiki ilitokana na kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977 wakati ambapo
chuo kilikuwa kikifahamika kama ‘Training School’. Mara baada ya kuvunjika kwa Jumuiya jina la chuo lilibadilishwa kutoka hilo la awali na kuwa ‘Bandari College – Dar es Salaam’ na kilihama kutoka Mtaa wa Sokoine kwenda Mtaa wa Tandika mwaka 1980.