Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, Mhandisi Deusdedit Kakoko (wa kwanza kushoto) akiongea na Waandishi wa Habari kuhusiana na maadhimisho ya 13 ya TPA. Wengine ni Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi ya TPA (katikati) na Bi. Francisca Muindi (wa kwanza kulia)

Na Mwandishi Maalum

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (Tanzania Ports Authority – TPA) inaadhimisha miaka 13 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005. TPA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 17 ya mwaka 2004 kwa kurithi kazi za iliyokuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (Tanzania Harbours Authority – THA) ambayo ilianzishwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambayo ilikuwa inaendesha bandari kupitia Shirika la Bandari la Afrika Mashariki (East African Harbours Corporation) ambalo lilianzishwa mwaka 1967.

THA ilikuwa na kazi ya kusimamia na kuendesha bandari za mwambao wa bahari tu ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Bagamoyo, Mafia, Pangani, Lindi na Kilwa. TPA ambayo ilianza rasmi kufanya kazi tarehe 15 Aprili, 2015 ilikasimiwa kazi ya kuendeleza na kusimamia bandari zote za mwambao wa Bahari ya Hindi na za kwenye Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Pia TPA ilikabidhiwa majukumu zaidi ya kumiliki na kuendeleza bandari zilizokuwa zinaendeshwa na Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Services Company Limited – MSCL) katika Maziwa Makuu.  Majukumu mengine ni pamoja na kuendeleza shughuli za bandari, kutangaza huduma za bandari, kushirikisha na kusimamia sekta binafsi katika uendelezaji, uboreshaji na uendelezaji wa bandari za mwambao wa bahari na za kwenye Maziwa Makuu nchini.

Kwa muda wa miaka 13 TPA imeendelea kuhudumia wateja wake katika bandari zake kwa kuwapatia huduma bora. Huduma hizo ni pamoja na za kuhudumia meli ambapo TPA imeendelea kuboresha miundombinu ya magati na kuwa na marubani wa kuongoza meli wenye ujuzi na uzoefu mkubwa. Pia kuwajengea uwezo wafanyakazi wengine wanaohusika na uhudumiaji wa meli wakati wa kuingia na kutoka bandarini. Pia TPA imefanikiwa kupunguza muda wa kukaa meli bandarini kwa kuongeza ufanisi kwa kushirikiana na wadau wa bandari kama vile idara za Uhamiaji na Afya.

Kwa upande wa kuhudumia mizigo ya wateja TPA imeboresha kwa kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili waweze kuhudumia wateja kwa kuwapatia huduma bora. TPA imeweza kuzinunulia bandari zake vifaa bora na vya kisasa vya kuhudumia meli na mizigo ya wateja. TPA kwa kushirikiana na wadau wake imefanikiwa kutoa huduma kwa wateja wake kuchukua mizigo yao bandarini kwa muda wa saa 24 kwa siku 7 za wiki. TPA imefanikiwa kuwawezesha wateja kulipia tozo za bandari kwa kutumia mfumo wa E-payament.

Ili kuweza kuhakikisha TPA inaendelea kutoa huduma bora katika bandari zake, iliamua kuwekeza katika miradi mikubwa kuboresha na kuendeleza bandari zake kukabiliana na changamoto ya ongezeko la shehena na kuweza kuingiza meli kubwa katika bandari zake.

Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, TPA imeweza kukamilisha miradi mingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Boya la Mafuta (Single Point Mooring – SPM) kuhudumia meli kubwa za mafuta zenye uwezo wa kuchukua mafua hadi tani 150,000. Ujenzi wa Kituo Kimoja cha Huduma (One Stop Centre), Mradi wa kisasa wa ulinzi (Integrated Security System), ujenzi wa barabara za kuingia lango namba 4 na 8 na ujenzi wa karakana ya meli (Dock Yard).

Mradi mkubwa unaotekelezwa katika bandari ya Dar es Salaam ni Dar es Salaam Maritime Gateway Project ambao ni mradi wa uboreshaji na uongezaji wa kina katika gati namba 1 hadi 7, kuongeza kina cha mlango wa bandari na mzunguko wa kugeuza meli pamoja na kujenga gati namba 13 na 14.

Katika bandari ya Mtwara, TPA imeongeza gati namba 2 kuipanua bandari hiyo kuwa ya kisasa kwa lengo la kuiwezesha kuhudumia meli kubwa na shehena kubwa zaidi. Mradi huo una lengo la kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mikoa ya Mtwara, Lindi and Ruvuma. Pia taifa kwa ujumla litanufaika kwa kuwapatia fursa wateja kuteremshia mizigo yao katika bandari hiyo. Mradi huo uliwekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Machi, 2017.

Katika Bandari ya Tanga, TPA imeongeza kina cha gati meli ziweze kufunga moja kwa moja gatini badala ya kufunga majini na mzigo kuletwa gatini kwa kutumia matishari hali inayomuongezea mteja gharama za upakuaji wa mzigo. Pia katika Bandari ya Tanga Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na Serikali ya Uganda kujenga bomba kubwa la mafuta la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kupitia Bandari ya Tanga. Mradi huu upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na unakwenda sambasamba na mradi mwingine wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani Tanga.

Aidha, TPA inaendelea na na uboreshaji wa miundombinu ya bandari zilizoko katika Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Bandari hizo zimejengewa na zinaendelea kujengewa uwezo kuhudumia meli, abiria na mizigo ya wateja. Pia ili kuhudumia mizigo ya wateja vizuri TPA inatekeleza mradi wa Bandari Kavu ya Kwala, Ruvu, ambapo imenunua maeneo ya Katosho Kigoma kwa ajili ya mizigo ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na eneo la Fela, Misungwi kwa ajili ya mizigo ya Uganda.

Ili kusogeza huduma za bandari karibu na wateja wake, TPA imefungua ofisi zake; Lubumbashi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lusaka nchini Zambia, Kigali nchini Rwanda na Bujumbura nchini Burundi. Pia, TPA ina mawakala Goma nchini Congo, Kampala nchini Uganda na iko mbioni pia kumpata wakala nchini Malawi.

Kwa muda wa miaka 13, TPA imepata mafanikio mengi ya kujivunia katika bandari zake ambayo yamechangia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania na nchi jirani zinazotumia bandari za TPA. Aidha TPA kwa kushirikiana na wadau wake itaendelea kuboresha utoaji huduma kwa wateja wake kwa kuwajengea uwezo wafanyakazi wake, kuboresha miundombinu pamoja na vifaa, kuendelea kutoa huduma bora kwa haraka na gharama nafuu kwa kutumia mifumo ya kisasa kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

TPA kwa kumjali mteja ina kituo cha huduma kwa mteja ambacho kina simu ambazo mteja anaweza kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi bure kuuliza swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047.