Bandari ni lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi zote zinazotumia bandari zetu hususan Bandari ya Dar es Salaam ambazo; ni Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan Kusini na Comoro.
Kutokana na umuhimu wa bandari katika nyanja za kiuchumi na kibiashara kwa nchi hizo, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa ikiboresha huduma zake kila wakati kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wateja wake zina ubora wa kiwango cha kimataifa.
TPA kwa kutambua umuhimu na thamani kubwa ya mteja katika utoaji wa huduma zake, inazingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja (Customer Service Charter) na imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Customer Service Center). Mambo haya yote yanaifanya TPA kuwa mtoa huduma bora anayemjali mteja wake wakati wote.
Mkataba wa Huduma kwa Mteja
Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni ahadi ya TPA na wateja wake ya kutoa huduma bora katika bandari zake. Mkataba huu ambao umeandikwa kwa lugha za Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa unaonyesha dhamira ya dhati ya TPA ya kuwahudumia wateja wake kwa heshima na kwa haraka bila ya upendeleo. Ni wajibu wa wateja wa TPA kuelewa kiwango cha huduma kinachotolewa na Mamlaka kwao. Endapo TPA inashindwa kutimiza matarajio ya wateja wake na kukiuka viwango ilivyojiwekea, ipo tayari kupokea maoni ya kurekebisha au kuboresha zaidi huduma zake.
Mkataba huu wa huduma kwa mteja unaitaka TPA kutoa huduma za bandari kwa ufanisi kuendana na mahitaji ya kibiashara ambayo yanazingatia ubora wa huduma, kwa kutumia nyenzo na miundombinu imara ili kutimiza mahitaji ya wateja. TPA imeahidi kutimiza ahadi yake kwa kufanya kazi kama timu kuboresha huduma kwa mteja na kuanzisha uhusiano wa kikazi wenye tija na watoa huduma za bandari kuhakikisha uwepo wa manufaa baina ya TPA na wateja wake.
TPA imedhamiria kwa dhati kutoa huduma kwa kiwango cha ubora wa kimataifa za uongozaji meli kuingia na kutoka bandarini, kuvuta meli bandarini, kutia na kung’oa nanga, msaada wa uongozaji wa vyombo baharini, utunzaji wa njia za majini/ mkondo wa kugeuzia meli, huduma za upakuaji, upakiaji na utunzaji mizigo bandarini na huduma kwa abiria wanaosafiri na meli.
Ili kufikia huduma za wateja zenye tija na ufanisi, bandari zinatoa huduma zake saa ishirini na nne siku saba kwa wiki (24/7), zinashughulikia mawasiliano kutoka kwa wateja; maulizo kwa taarifa za kawaida mteja atajibiwa katika wastani wa dakika tatu nyakati za saa za kuanzia saa 1:30 asubuhi mpaka saa 10:30 jioni.
Maulizo kuhusu uendeshaji/ masoko/ biashara mteja atajibiwa ndani ya saa 24 baada ya kupokea maulizo yake, maandishi au kero mteja atajibiwa katika muda wa siku saba (7) baada ya kupokea barua yake na kumshauri hatua inayotarajiwa kuchukuliwa na tarehe ya hatua hiyo. Majibu ya maulizo kwa njia ya barua pepe na fax mteja atajibiwa ndani ya muda wa saa 24. Iwapo kuna mabadiliko yoyote kuhusiana na muda wa kuchukua hatua mteja atafahamishwa.
Utambulisho wa wafanyakazi wa TPA wakiwa kazini uko wazi, kwani wanatambulika kwa vitambulisho vyenye majina yao, jina la idara zao na namba zao za kazi. Ndani na nje ya bandari za TPA, kuna alama za usalama zinazoeleweka, zenye maelekezo mbalimbali yaliyobandikwa na kusomeka kwa urahisi. Kwa upande wa ulinzi ni jukumu la TPA kuhakikisha ulinzi na usalama katika utoaji wa huduma bandarini na mazingira ya kazi yenye ulinzi na usalama wakati wote.
Katika mkataba wake wa huduma kwa mteja, TPA inahakikisha mteja anahudumiwa kwa ukarimu. Pia kama mteja aliweka miadi kabla, TPA inamhudumia mteja katika idara zinazohusika ndani ya muda wa dakika 15, vinginevyo kama kuna shida ufumbuzi upatikane ndani ya dakika 30. Ni ahadi ya TPA kumhudumia mteja wake kwa heshima stahiki na kuhakikisha kero zinazojitokeza zinashghulikiwa kwa haraka na uadilifu.
TPA katika kumjali mteja wake, inathamini na kukaribisha maoni na mapendekezo kuhusu huduma zake zenye lengo la kusaidia kuboresha huduma zake. Mteja anayo haki ya kuwasiliana na TPA kwa kufika, kupiga simu, kuandika barua pepe n.k; ili aweze kuhudumiwa vizuri na kwa haraka. Pia mteja anayo haki za kuuliza au kulalamika asiporidhishwa na kiwango cha huduma alizopata, kukata rufaa kuhusu suala lolote linalohusu huduma zisizopatiwa ufumbuzi kwa mamlaka za juu, kuhudumiwa kwa heshima na kuzingatia usahihi katika miamala yake na TPA. Pia mteja ana haki ya kupata huduma za TPA zenye ufanisi na ubora bila rushwa wala hongo.
Aidha, ili mteja kuhudumiwa vizuri, TPA inatarajia kutoka kwa mteja; taarifa sahihi, kwa wakati na nyaraka kamili, heshima na kuwathamini wafanyakazi wa bandari, kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika miamala yake na TPA, kutoa maoni kuhusu huduma alizopata, kupendekeza namna ya kuboresha huduma za bandari na kujaza fomu za maoni kwa njia ya barua pepe.
Kituo cha Huduma kwa Mteja (Customer Service Center)
TPA imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja ndani ya Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea na kujibu kero/ malalamiko ya wateja kwa njia ya simu za bure za TPA kwa wakati kuhusiana na huduma za bandari. Simu hizo ni 0800110032 au 0800110047. Kituo hiki kinatoa mawasiliano na taarifa ndani na nje kwa njia ya machapisho mbalimbali zenye taarifa za TPA. Ni kituo cha kutoa ushauri juu ya uagizaji na usafirishaji wa mizigo. Pia kituo kinachotunza kumbukumbu za wateja na wadau wa bandari.
TPA inapenda kuwahakikishia wateja wa ndani na nje kwamba bandari zake zitaendelea kutoa huduma kwa kiwango chenye ubora wa kimataifa. Pia TPA inaahidi kuendelea kuboresha ulinzi na usalama kwa mizigo ya wateja wake kuwa wa kisasa kila wakati.