Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imefanya mambo mengi katika utoaji huduma bora kwa wateja wake. Ili kuhakikisha TPA inawahudumia wateja wake vizuri iliamua kuwa na Mkataba wa Huduma kwa Mteja, kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Wateja na kufungua Dawati la kushughulikia malalamiko ya wananchi.
Ndugu msomaji, katika makala hii tunakujulisha hatua ambazo mteja anapaswa kuchukua iwapo mzigo wake utapotea au kuharibika ukiwa mikononi mwa TPA. Pia makala hii itakufafanulia utaratibu wa minada kwa mizigo iliyokaa muda mrefu bandarini.
Mzigo wako ukipotea au kuharibika bandarini unafanyaje?
TPA imeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia matatizo ya wateja. Iwapo mzigo wa mteja utakuwa umeharibika au umepotea ukiwa mikononi mwa TPA, basi mteja atatakiwa kuandika barua ya kueleza kwamba mzigo wake umeharibika au umepotea ukiwa mikononi mwa Bandari. Baada ya kuipokea barua hiyo, TPA itafanya uchunguzi kubaini ukweli wa kile kilicholalamikiwa na mteja.
Uchunguzi ukishafanyika mteja atafahamishwa au kujibiwa kulingana na matokeo. Iwapo itagundulika kwamba mzigo wa mteja haujaharibika au kupotea ukiwa mikononi mwa Bandari, mteja atajulishwa kwa maandishi kwamba TPA haiusiki na uharibifu au upotevu wa mzigo wake.
Iwapo uchunguzi utabaini kwamba mzigo wa mteja umeharibika au kupotea ukiwa mikononi mwa TPA, basi mteja atapewa fomu maalum ambayo atatakiwa kuijaza kuwasilisha madai yake halisi kwa kuonyesha kiwango au gharama ya uharibifu. Madai hayo baada ya TPA kuyapokea, itafanya uhakiki kujiridhisha iwapo gharama iliyowasilishwa ni sahihi, na endapo itaonekana madai ni ya kweli, TPA itamlipa mteja gharama ya uharibifu au upotevu wa mzigo wake au upungufu wowote uliotokea.
Muda wa kuwasilisha madai
Madai ya mteja yatatakiwa yawasilishwe ndani ya miezi sita tangu mzigo husika ulipowasili bandarini. Lengo la kufanya uchunguzi ni kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili kwa TPA na mteja pia. Endapo mteja atakuwa hajaridhika kwa jinsi madai yake yalivyoshughulikiwa na TPA, anayo fursa ya kukata rufaa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).
Muda wa mzigo kukaa bandarini, kunadiwa
Makala hii inaelezea utaratibu wa minada unaofanywa kwa mizigo ya wateja. Kwa upande wa Bandari, mteja anawajibika kulipia mzigo wake tozo mbalimbali za bandari ‘port charges’ kama tulivyoona kwenye makala zilizopita. Kwa mizigo ya hapa nchini, endapo mteja atauchukuwa mzigo wake bandarini ndani ya siku 7 baada ya meli kushusha mzigo wake au siku 15 kwa mzigo unaosafirishwa nje ya Tanzania, mteja hatatozwa gharama ya pango (storage charges) ya mzigo wake. Kama mzigo wa mteja utakaa bandarini zaidi ya siku hizo, basi mzigo huo utatozwa gharama za pango kwa viwango mbalimbali kwa siku, kutegemeana na aina ya mzigo kama ilivyoainishwa kwenye kitabu cha tozo za TPA maarufu kama ‘tariff book’ ambacho kinapatikana kwenye tovuti ya TPA www.ports.go.tz.
Aina za minada
TPA tumekuwa tukiwasisitiza wateja kuhakikisha wanaanza kushughulikia nyaraka za uondoshaji mizigo mapema hata kabla ya meli kuingia bandarini kuepuka gharama za tozo la pango. Kwa mzigo uliokaa bandarini kwa siku 21, utakuwa umeingia kwenye hatari ya kupigwa mnada kulingana na sheria zilizopo na TPA itaukabidhi mzigo huo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kwa ajili ya utaratibu wa kupigwa mnada.
Kuna aina mbili za minada kwa mizigo ya wateja iliyokaa bandarini zaidi ya siku 21. Aina ya kwanza ni mnada unaofanywa na TRA. Mnada huu ufanyika endapo mteja atashindwa kulipia kodi ya Serikali kwa TRA na tozo za bandari.
Aina ya pili ni mnada unaofanywa na TPA. Mnada unafanywa na TPA kwa mzigo ambao mteja atakuwa amelipia kodi ya Serikali kwa TRA, lakini ameshindwa kulipia tozo za Bandari kwa TPA. Kabla minada hiyo haijafanyika Mamlaka husika wanatakiwa kutangaza kwenye vyombo vya habari kwa kuorodhesha mizigo ya wateja iliyokaa bandarini zaidi ya siku 21. Kupitia matangazo hayo wateja wanapewa siku za kulipia na kutoa mizigo yao, endapo watashindwa kufanya hivyo Mamlaka husika yani TRA au TPA wanapiga mnada mizigo hiyo. Minada yote hufanyika kwa uwazi watu wengi waweze kushiriki.
Ili mizigo isipigwe mnada, wateja wanashauriwa kulipia mizigo yao mapema mara tu baada ya kupata nyaraka zao za bill of lading kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza. TPA wakati wote itaendelea kuboresha utoaji huduma kwa wateja wake. Endapo una swali lolote unaweza kutuma ujumbe au kupiga simu za bure kupitia namba za simu 0800110032 au 0800110047.