Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na wadau wake wa bandari imeboresha na kurahisisha upakiaji, upakuaji na utoaji wa mizigo katika bandari zake.
Uboreshaji huo umefanyika na unaendelea kufanyika kwa sababu bandari ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi zote zinazotumia bandari za TPA, hususan Bandari ya Dar es Salaam.
Kati ya mambo yaliyoboreshwa na yaliyorahisishwa katika utoaji wa huduma kwa wateja ni pamoja na bandari kwa kushirikiana na wadau wake kufanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki, maarufu kwa 24/7.
Utendaji kazi huu wa wadau ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, ambapo aliwataka wadau wote wa bandari kufanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki ili kuharakisha utoaji wa mizigo bandarini.
Maagizo hayo yalitolewa kwa kuwa utendaji wa bandari wenye ufanisi utasaidia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania na nchi zote zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam. Vilevile itasaidia katika kuondoa changamoto zilizokuwa zinawakabili wateja wa bandari wakati wa uagizaji au uondoshaji wa mizigo kutoka bandarini.
Wateja wanatakiwa kuitumia fursa ya bandari kufanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki kuchukua mizigo yao pindi inapowasili tu bandarini kuepuka gharama za kulipia pango (storage charges) kwa mizigo yao.
Endapo mteja atauchukua mzigo wake bandarini ndani ya siku saba kwa mzigo wa hapa nchini na siku 15 kwa mzigo wa nchi zinazotumia bandari zetu, mteja hatatozwa gharama ya pango ya mzigo. Kama mzigo wa mteja utakaa bandarini zaidi ya siku hizo, basi mzigo huo utatozwa gharama za pango.
Ni vizuri wateja wa bandari wakafahamu kwamba ndani ya bandari kuna matawi mawili ya Benki ya TIB na NMB, ambayo yapo wazi wakati wote, hivyo wasiwe na wasiwasi juu ya sehemu ya kulipia tozo za bandari (port charges) wanapotaka kuchukua mizigo yao.
Wadau wote kwa pamoja wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kulingana na maagizo ya Serikali. Kila mdau anatakiwa kuwafahamisha wateja kwamba bandari inafanya kazi kwa saa 24 kwa siku 7 bila kupumzika, hivyo wateja wanatakiwa kuitumia fursa hiyo ilete tija kubwa na ufanisi katika utekelezaji wake.
Kabla ya mpango huu kuanza, TPA imekuwa ikifanya kazi kwa muda wa saa 24 kwenye maeneo ya upakiaji na upakuaji wa mizigo, lakini wadau wengine wa bandari walikuwa wanafanya kazi kuanzia saa 1:00 asubuhi mpaka saa 12:00 jioni. Ufanyaji kazi huo ulichangia kuchelewesha shughuli za usafirishaji na uondoshaji wa mzigo bandarini.
Kutokana na hilo, ndiyo maana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli iliona bandari ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, wenye tija, kuna umuhimu kwa wadau wote wa bandari wafanye kazi kama TPA. Lengo ni kuhakikisha wateja wanapata wigo mpana na fursa kubwa zaidi ya kusafirisha au kuchukua mizigo yao bandarini muda wowote wa mchana au usiku.
Usafirishaji kwa njia ya maji ni njia rahisi za usafirishaji ambao ukitumika vizuri unaweza kurahisisha shughuli za kusafirisha au kuagiza mizigo kwenda na kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa urahisi zaidi.
Nchi ya Tanzania kijiografia imebahatika, kwani imezungukwa na maji ya bahari na maziwa kuliko nchi yoyote Afrika. Kwa kutumia usafirishaji kwa njia ya bahari na maziwa, wasafirishaji wa shehena kubwa za mizigo wanapata fursa ya kusafirisha mizigo yao kwa gharama nafuu na kwa wepesi sana.
Fursa hii ya kuwa na bandari kubwa hasa ya Dar es Salaam ambayo inatumiwa na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Sudan ya Kusini na Visiwa vya Komoro ni muhimu sana kwa wadau wa bandari kufanya kazi kwa saa 24 kwa siku zote za wiki, kwa lengo la kuwawezesha wateja kuchukua shehena kubwa ya mizigo bandarini ili kuepuka ucheleweshaji wa utoaji mizigo ambao unaweza kusababisha gharama kubwa kwa wateja.
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo kwenye kampeni ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi imara wa viwanda, hivyo bandari pamoja na wadau wake wana mchango mkubwa wa kuisaidia Tanzania kufikia lengo hilo. Hatua hiyo inaweza kufanikiwa iwapo tu wadau wa bandari watatimiza wajibu wao kwa kufanya kazi yenye tija na ufanisi mkubwa.
Ufanisi wa bandari utawezesha bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa kusafirishwa bila vikwazo na hata malighafi zitakazokuwa zinahitajiwa na viwanda nchini zitakuwa zinawafikia wenye viwanda kwa wakati mwafaka. Uchumi wa viwanda utaiwezesha Tanzania kupata maendeleo makubwa na ustawi wa maisha ya watu wake.
Kama unataka ufafanuzi zaidi kuhusiana na mpango huu wa bandari na wadau wake kufanya kazi saa 24 kwa siku 7 za wiki au una swali lolote kuhusiana na huduma zinazotolewa na bandari unaweza kutuma ujumbe au kupiga simu za bure za TPA kwa kutumia namba 0800110032 au 0800110047 na utapata ufafanuzi au majibu kwa maswali yako.