Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

AFISA Uhusiano wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC), Ezekiel Nyalusi amesema ni vyema jamii ikafahamu haki na wajibu wa mteja au mgonjwa pindi anapofika kupewa huduma za Afya katika kituo cha kutolea huduma.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Nyalusi ameziainisha haki hizo kuwa ni kupatiwa taarifa anazohitaji mgonjwa kuhusu ugonjwa na matibabu yake, kupatiwa matibabu bila kukemewa, kukaripiwa au kufedheheshwa, Kupata huduma kwa wakati, kutegemea aina ya huduma.

“Haki nyingine ni kuwa na hiyari kupata taarifa za kiafya, kupata huduma stahiki kwa makundi maalumu kama vile, Walemavu, Wazee, Wajawazito, Watoto wa chini ya miaka mitano na wenye magonjwa sugu.

“Pia kulalamika au kutoa mrejesho wa huduma uliyopatiwa, kufuata kanuni na taratibu za kituo husika, kuwaheshimu watoa huduma ikiwa ni pamoja na kutumia lugha Safi, kumueleza muhudumu wa Afya taarifa zote ambazo zitamuwezesha kutoa tiba sahihi ikiwa ni pamoja na kumpa rekodi za matibabu ya awali alizonazo magonjwa,” amesema.

Amebainisha kuwa haki nyingine ni kutafuta matibabu kwa haraka na mapema iwezekanavyo ili wahudumu wa Afya waweze kutoa huduma sahihi.

Naye Msajili kutoka Baraza hilo, Agnes Mtawa amesema kuwa ili waweze kutoa huduma iliyobora wauguzi na wakunga ni lazima wazingatie msingi saba ya maadili yao.

Mtawa ameitaja na kufafanua misingi hiyo ambapo amesema ni lazima waheshimu utu, mila na desturi na kwamba wanapomhudumia magonjwa wamuhudumie kama yeye na sio kumlinganisha na mtu mwingine.

“Msingi mwingine ni lazima muuguzi, mkunga apate idhini ya mteja kabla ya kutoa huduma, magonjwa aelezwe anapata huduma gani na msingi wa tatu ahakikishe anawajibika na kile anachokifanya kama anampa dawa ahakikishe anafuata taratibu ili chochote kinachotokea awajibike mtoa huduma na si mtu mwingine,” amesema Msajili huyo.

Amesema kuwa msingi wa nne ni lazima muuguzi, Mkunga afanye kazi kama timu ili magonjwa aweze kutibiwa na timu hiyo na kwamba msingi wa tano mtoa huduma atunze siri za magonjwa asiwe chanzo cha magonjwa huyo kushindwa kupata huduma.

Mtawa ameongeza kwamba msingi wa sita lazima muuguzi,mkunga awe tayari kujiendeleza kitaalamu kwa kuwa taaluma ya mambo ya afya inabadilika kila siku.

Amesema kuwa msingi wa saba muuguzi, mkunga anapaswa kuwa mwaminifu kutoa huduma bila upendeleo wa kuangalia rafiki,kabila na rangi ili kuleta usawa katika kuhudumia wagonjwa.