Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kikundi kazi cha Baraza la Biashara nchini (TNBC) kwa ajili ya kuangalia fursa za kiuchumi zitakazopatikana kupitia Uchumi wa Buluu kimezinduliwa jijini Dar es Salaam, huku wajumbe wa kikundi hicho kutoka sekta sekta binafsi wakielezea matumaini yao ya uchangiaji wake katika ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha kikundi hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw.Abdallah Mitawi amesema kuwa kikundi kazi hicho ni muhimu katika kuangalia maeneo ambayo uchumi wa Buluu utasaidia katika kukuza uchumi hapa nchini na kuchangia katika pato la taifa.

Amesema utekelzaji wa mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya mkutano wa Dunia uliofanyika mwaka 2012 Rio de Janeiro, Brazil na ule wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mwaka 2019 ambayo kwa pamoja iliangalia mchango wa uchumi wa buluu katika kukuza uchumi barani Afrika kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo bahari, mito, maziwa vyenye aina mbalimbali ya samaki na viumbe wengine na mazao yanayotokana na vyanzo vya maji.

Amesema kwa upande wa Zanzibar, utekelezaji huo ulianza mwaka 2019 na tayari umepiga hatua mbalimbali ikiwemo kuanzisha Wizara maalum inayojishughulisha na uchumi wa buluu.

Ameongeza kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, sera ya uchumi wa Buluu tayari imeanzishwa mwaka huu na kinachofuata ni uratibu wake, ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira ndio yenye jukumu la kikatiba la kuratibu jambo hili.

Amesema utekelezaji wa Uchumi wa Buluu ni sekta mtambuka inayojumuisha sekta nyingine mbalimbali ikiwemo uvuvi, madini, maliasili na utalii, nishati, viwanda na biashara, uhifadhi wa mazingira, uwekezaji na umwagiliaji.

“Tumekutana ili kuangalia fursa na changamoto katika azimio hili na kuja na mapedekezo mbalimbali katika kuhakikisha sekta hii inachangia kwa kiasi kikubwa kupitia michango ya sekta nyingine hapa nchini”amesema.

Akichangia mada katika kikao hicho, Ambrose Mugisha, Mkuu wa Kitengo cha Uchumi wa Buluu kutoka Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) amesema kuwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) limetabiri kuwa katika miaka 10 ijayo, uchumi wa Tanzania utakuwa mara mbili zaidi ya sasa na kuwa kinara katika Afrika ya Mashariki kupitia fursa mbalimbali ikiwemo sekta ya uchumi wa Buluu kutokana na upatikanaji wa vyanyo mbalimbali ikiwemo bahari,mito na maziwa.

Amesema kwa kipindi hicho, idadi ya watu hapa nchini inakadiriwa kufikia milioni 100 ambao kwa kiasi kikuwa watakuwa kiungo muhimu iwapo mipango mizuri ya utekezaji wake itapangwa.

Hii inatokana na takwimu za IMF kuwa katika miaka 10 au 15 ijayo, uchumi utakaokuwa unakuwa kwa kasi zaidi duniani ni wa uchumi wa buluu na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alitembelea nchi mbalimbali ikiwemo Korea na kuangalia maeneo ya ushirikiano kupitia uchumi wa buluu.

Naye Lamine Diallo, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili kutoka Umoja wa Ulaya (EU) amesema kuwa umoja huo umekuwa ukifadhili shughuli mbalimbali zinazohusiana na uchumi wa buluu hapa nchini ili kuchochea ukuaji wake kwa haraka.

Ufadhili huo ni wa miradi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ikiwemo uvuvi na mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Katibu Mtendaji wa (TNBC), Dkt. Godwill Wanga alisema miongoni mwa mambo waliyojadiliana na kukubaliana ni pamoja na kuboresha mazingira yote yanayohusu uchumi wa buluu.

“Tumekubaliana kuangalia maeneo kadhaa ikiwemo yale yatakayosaidia ukuaji wa haraka wa uchumu kupitia sekta hii,” amesema.

Dkt. Wanga aliwashukuru wadau wa Maendeleo wakiwemo EU, UNDP na wadau wengine wa sekta binafsi na kuwaomba waendelee kujitolea kwa ajili ya kusaidia ukuaji wa uchumi wa buluu hapa nchini katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia.