Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewataka wakaguzi wa viwanda vya kutengeneza dawa kufuata maadili kwani wao ndio nguzo kubwa katika kuhakikisha dawa zinazozalishwa zinakidhi vigezo vya kitiba na kiuchunguzi.
Wito huo umetolewa leo Desemba 15,2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA Adam Fimbo, wakati akizngumza na waandishi wa habari kuhusu mafunzo ya siku tano kwa wakaguzi wa viwanda wa taasisi hiyo.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa wakaguzi hao katika kuhakikisha wanasimamia ubora wa dawa wameamua kuwapa elimu hiyo ili kuhakikisha viwanda vinatengeneza bidhaa zenye viwango ili kuepusha kuingiza bidhaa duni sokoni ambazo zitaleta athari kwa jamii.
“Sisi kama TMDA kazi ya ukaguzi ni kazi yetu ya msingi hivyo tunafanya ukaguzi kwenye viwanda vinavyotengeneza dawa ili kuhakikisha jamii haipati madhara yanayotokana na dawa zisiszokidhi viwango kwa matumizi ya binadamu.” amesema Fimbo.
Amesema TMDA ina jumla ya wakaguzi 45 hivyo wanahitaji wakaguzi zaidi ili kuendelea kufanya kazi hiyo kwa ufanisi ingawa wakaguzi waliopo wanaweza kufikia sehemu zote.
“TMDA tunakagua viwanda,maduka ya jumla na rejereja na maghala hivyo ni lazima tuwe na wakaguzi wa kutosha kwani mpaka sasa wapo 45 kwa asili ya kazi yetu haina shida sana lakini tunahitaji tuwapate wa kutosha zaidi ili watusaidie kufanya ukaguzi”amesema.
Ameongeza kuwa uwepo wa kaguzi hizo umesaidia viwanda hasa vya ndani kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyohitajika nchini.
Kwa upande wake mmoja wa wakaguzi ambao wapo kupata mafunzo hayo Bugusu Mweru ambaye ni Mkaguzi na Mchambuzi wa Maabara kutoka Kanda ya Ziwa amesema mafunzo hayo yatawasaidia kwenye kaguzi zao ili kuhakikisha jamii inapata dawa zenye ubora na zilizokidhi vigezo vya kitiba.
Mafunzo hayo ya siku tano yaliyowakutanisha wakaguzi 34 yanalengo la kuwasaidia wakaguzi kufanya kazi zao kwa weledi na maadili na kukwepa vitendo vya rushwa kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.