MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao lililopo katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ili kuweza kujifunza mambo mbalimbali hasa matumizi sahihi ya dawa.
Wito huo umetolewa na Meneja TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
“Tumekuja kwenye maonesho haya kuwaelimisha wananchi na kazi za TMDA…ambapo kazi yake kubwa ni kuhakikisha tunadhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa, vifaatiba na vitenganishi ili bidhaa hizi zinapoenda kutumika kwa wananchi hata wagonjwa ziwe salama, fanisi na zenye ubora unaotakiwa.
“Na ili tuweze kuhakikisha huo usalama na ufanisi unatimilika, kuna majukumu ambayo mamlaka inayafanya ikiwemo kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zimesajiliwa na hata zile zinazozalishwa katika viwanda vyetu na zenyewe ziwe zimesajiliwa,” amesema.
Amefafanua kuwa TMDA pia inahakikisha nyaraka zote zenye usajili na bidhaa zinapimwa kama zimezingatia vigezo na kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia kwenye soko zina ubora unaotakiwa, usalama na ufanisi.
“Kushiriki katika maonesho haya tumekuja kutoa elimu mbalimbali hususani ya matumizi sahihi ya dawa, jinsi ya kutupata na kama una malalamiko pia tunapokea ili kusudi tuweze kufanya huduma bora zaidi na Watanzania waweze kuwa na afya njema.
“Tunatoa rai kwa wananchi kuweza kutembelea maonesho hayo, ili tuwaelimishe na waache matumizi ya dawa kiholela,” amesema.