Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Ziwa Mashariki, imeonya juu ya matumizi mabaya ya dawa za kuzuia ujauzito na kuongeza nguvu za kiume, ambayo yamebainika kuhatarisha afya za watumiaji.
Onyo hilo limetolewa na Mkaguzi wa Dawa wa TMDA, Benson Katundu, alipokuwa akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bunda na Chuo cha Kisangwa FDC, kilichopo Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara.
Katundu alieleza kuwa baadhi ya watoto wa kike wanatumia dawa za kuzuia mimba bila kufuata ushauri wa kitaalam, hali inayoweza kusababisha madhara makubwa kiafya. Aidha, aliwataka vijana wanaotumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kuacha mara moja, kwani matumizi hayo si salama na yanaweza kuhatarisha maisha yao.
Elimu hii ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kuongeza Uelewa kuhusu Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA), inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 18 hadi 24. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Elimisha, Hamasisha, Chukua Hatua Sasa”. TMDA inaendelea kutoa elimu katika shule, minada, na maeneo mengine ya jamii ili kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa na kupambana na changamoto za usugu wa vimelea vya magonjwa.
Kwa ujumla, TMDA imesisitiza umuhimu wa kuzingatia ushauri wa kitaalam kabla ya kutumia dawa yoyote ili kulinda afya na usalama wa maisha.