Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), imetoa angalizo ya siku mbili  ya kunyesha kwa mvua kubwa  kwa baadhi ya maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani (Visiwa vya Mafia ,Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, leo Juni 5, 2023 jijini Dar es Salaam na imeonyesha matarajio ya kunyesha kwa siku tano ambapo kati ya tarehe Juni 6 na 7 mwaka huu kutakuwa na mvua na pia Juni 8 na 9 mwaka huu kunaonyesha kuwepo kwa mvua kubwa katika maeneo hayo.

Taarifa hiyo ilisema  kuna uwezekano wa kutokea kwa wastani kiwango cha athari zinazoweza kujitokeza kipindi cha mvua hizo kunyesha katika maeneo hayo ikiwemo makazi kujaa maji pamoja na kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi.

Aidha TMA imetoa tahadhari kwa wananchi kuendelea kufuatilia utabiri unaotolewa na mamlaka hiyo ili kuweza kuchukua tahadhari mbalimbali.