Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA),imetoa tahadhari kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika bahari ya Hindi kuhakikisha wanachukua tahadhari kutokana na angalizo la kuwepo kwa vipindi vua upepo mkali.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa Hali ya Hewa kutoka TMA,Rose Senyagwa amesema kutakuwepo kwa vipindi vya upepo mkali unaofikia Kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia Mita 2.0 katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Amesema maeneo yanayotarajiwa kukumbwa na upepo huo ni pamoja na mikoa ya Lindi,Mtwara,Tanga,Pwani na ikijumuisha visiwa vya Mafia.
Amesema kuwa maeneo mengine ni Mkoa wa Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo hali hiyo inatarajiwa kujitokeza kuanzia leo Jan 20 hadi 23, mwaka huu.
“Athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuathiri shughuli za uvuvi na usafirishaji katika maeneo ya bahari ya Hindi’amesema Senyagwa.
Hata hivyo mamlaka hiyo imetoa tahadhari kwa wananchi wanaofanya shughuli zao katika bahari ya Hindi kuhakikisha wanachukua tahadhari katika kipindi hicho.